Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

BALOZI SALUM - MAONESHO YA SIDO NI JUKWAA MUHIMU KWA WAJASIRIAMALI KUTANGAZA BIDHAA ZAO.


📌Asema Maonesho hayo ni jitihada za kuendeleza ujasiriamali, kukuza viwanda vya ndani na kuimarisha uchumi.

Kahama, Shinyanga

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Waziri Salum amesema Maonesho ya SIDO Kitaifa ni jukwaa muhimu kwa wajasiriamali kutangaza bidhaa zao, kuonesha ujuzi na ubunifu wao, pamoja na kutafuta masoko mapya ya bidhaa wanazozalisha. 

Amesema hayo alipotembelea mabanda ya wajasiriamali wanaoshiriki Maonesho ya Kitaifa ya SIDO yanayofanyika katika Viwanja vya Magufuli, Kahama, mkoani Shinyanga, Oktoba 23,2026.

Balozi Salumu amesema maonesho hayo yanatoa fursa ya kujenga mahusiano ya kibiashara kati ya wazalishaji, wanunuzi na wadau wengine wa maendeleo, jambo linaloweza kusaidia kukuza biashara na kuongeza kipato cha wajasiriamali.

Aidha Balozi Salumu amewakaribisha wananchi kujitokeza kwa wingi kutembelea maonyesho hayo ili kujifunza,kutambua bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali
wa ndani, pamoja na kutumia fursa zilizopo kwa ajili ya kukuza biashara na shughuli za kiuchumi.

Ameongeza kuwa kama Serikali kupitia Wizara ha Viwanda na Biashara itaendelea kuongeza bajeti kwa SIDO ili kuendeleza umuhimu kuunga mkono juhudi za SIDO katika kuwajengea uwezo wajasiriamali, ili waweze kuboresha ubora wa bidhaa zao, kuongeza uzalishaji na kupanua masoko ndani na nje ya nchi. Ameeleza kuwa uwezeshaji wa wajasiriamali na uendelezaji wa viwanda vidogo ni miongoni mwa hatua muhimu za kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kuimarisha maendeleo ya viwanda nchini.