Kuhusu Wizara
Wizara ya Viwanda na Biashara imeundwa kwa mujibu wa Hati idhini GN Na. 619A ya tarehe 30 Agosti 2023. Wizara hii inatekeleza majukumu yake ya kimuundo kwa kuzingatia maelekezo ya Viongozi Wakuu wa Serikali, sambamba na mipango mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kama ilivyoainishwa kwenye Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs 2030); Agenda ya Afrika 2063; Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya Mwaka 2020; na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22-2025/26.
Pia, katika kuchochea kasi ya ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea kufanya mapitio ya Sera, Mikakati na Sheria za kisekta ili ziweze kuendana na mahitaji ya sasa. Sera hizo ni pamoja na Sera ya Taifa ya Uhamasishaji Uwekezaji (1996); Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda (SIDP, 1996 - 2020); Sera ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo (2003); Sera ya Masoko ya Mazao ya Kilimo (2003); na Sera ya Taifa ya Biashara (2003). Zoezi hilo linakwenda sambamba na kurejea Sheria na Mikakati ya kisekta ikiwemo Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Ngozi na Bidhaa za Ngozi; Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Pamba, Nguo hadi Mavazi (C2C); Mkakati wa Kuendeleza Zao la Alizeti; Sheria ya Kujilinda dhidi ya Athari za Kibiashara (Trade Remedies Act, 2021); Sheria ya Uwekezaji (1997) na Sheria ya Ushindani (2003).
Aidha, Wizara ipo katika hatua mbalimbali za uandaaji wa Sera mpya katika masuala ya ubora (National Quality Policy); miliki ubunifu (Patent Right Policy); ushiriki wa Watanzania katika miradi ya kimkakati na uwekezaji (Local Content Policy); na masuala ya kumlinda mlaji (National Consumer Protection Policy); na mikakati mipya ikiwemo Mkakati wa Kukuza Mauzo ya Nje (National Export Strategy).