Habari
CHUO CHA ELIMU YA BIASHARA CHATAKIWA KUTUMIA TAFITI KUCHOCHEA MAGEUZI YA KIUCHUMI KUELEKEA DIRA 2050
📌Asema mikutano ya kitaaluma inachochea mageuzi ya kiuchumi na ubunifu;
Mwanza
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb), amekitaka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kuhakikisha wanatumia tafiti kuchochea mageuzi ya kiuchumi kuelekea Dira 2050.
Amesema hayo wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Saba wa Kitaaluma wa Kimataifa wa Mwaka 2026 ulioandaliwa na Chuo cha CBE uliofanyika Mwanza.
Londo amesema mkutano huo unachochea mageuzi ya mifumo ya kibiashara, ubunifu, urasimishaji na matumizi ya takwimu kuelekea ukuaji endelevu wa uchumi ambapo inaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kutekeleza Dira ya Taifa ya 2050 kwa vitendo.
Mhe. Londo pia ametoa rai kwa Taasisi za Serikali na Sekta Binafsi kuanza kutumia kikamilifu matokeo ya tafiti kutoka vyuo vya elimu ya juu ili kuleta tija na matokeo chanya kwa maendeleo ya Taifa.
Aidha amekitaka Chuo hicho kuandaa changanuzi za kisera (policy briefs) zitakazosaidia maboresho ya sera na mipango ya kiuchumi na kuweka mikakati ya kurudisha mrejesho kwa jamii kwa kuwasilisha matokeo ya tafiti kwa lugha rahisi, kuendesha mafunzo maalumu kwa wajasiriamali na wafanyabiashara, na kutoa rai kwa vyuo vingine kuiga mfano wa CBE katika kuandaa mikutano ya kitaaluma.
Vilevile amekitaka Chuo hicho kuendelea kuboresha kozi zake za muda mfupi na mrefu ili kuzalisha wataalamu wa kutosha watakaofundisha somo hilo mashuleni na kuimarisha elimu ya biashara nchini kwa kuwa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2023 imefanya somo la Biashara kuwa la lazima kwa wanafunzi wa Kidato cha Kwanza hadi cha Nne kuanzia mwaka wa masomo 2025/2026.
