Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

KAPINGA ATOA WITO KWA VIJANA KUTUMIA FURSA ZA BIASHARA ZA MITANDAONI


📌Azindua jukwaa la CRDB intaprenyua 2026 kuwawezesha wajasiriamali kiuchumi;

📌Awataka wajasiriamali kulinda majina ya chapa zao kisheria

Dar es salaam

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amewataka vijana na wajasiriamali kutumia fursa za mitandao ya kijamii kukuza biashara zao, kuongeza kipato na kutengeneza ajira, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha mazingira wezeshi kwa biashara za kidijitali nchini.

Waziri kapinga ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam, wakati akifungua Jukwaa la CRDB Instaprenyua 2026 lililoandaliwa na Benki ya CRDB, ambapo amesema biashara za mitandaoni zimekuwa fursa muhimu zinazowawezesha wajasiriamali kufikia wateja na masoko bila kuhitaji eneo maalumu la kufanyia biashara.

Amesema serikali itaendelea kushirikiana na wadau kuboresha huduma na kuhakikisha teknolojia inakuwa daraja la kufikia fursa za kiuchumi badala ya kuwa kikwazo kwa maendeleo ya biashara, ameongeza kuwa ni muhimu kwa Watanzania kuhama kutoka matumizi ya kawaida ya teknolojia kwenda kwenye matumizi yenye tija yanayojenga biashara imara, zenye faida na uwezo wa kushindana katika masoko.

Aidha, amewataka wajasiriamali kusajili na kulinda majina ya chapa zao kisheria akisisitiza kuwa na wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii pekee hakutoshi kulinda chapa, huku akiwahimiza kutumia takwimu za oda, wateja na mauzo kupima mafanikio ya biashara badala ya kutegemea idadi ya likes na followers pekee.

Kapinga amesisitiza umuhimu wa kutunza kumbukumbu sahihi za mapato na matumizi, kutenganisha fedha za biashara na matumizi binafsi na kulinda faida ili kuimarisha biashara na kupunguza uwezekano wa kula mitaji, ambapo amewataka wajasiriamali kutumia teknolojia kwa ufanisi na uwajibikaji, huku wakichukua tahadhari dhidi ya utapeli na kulinda taarifa za wateja.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Benki ya CRDB, Mussa Kitambi, amesema benki hiyo itaendelea kuwawezesha wajasiriamali kupitia mafunzo ya usimamizi wa fedha, masoko, ujenzi wa chapa na matumizi ya majukwaa ya kidijitali, ameeleza kuwa huduma za benki hiyo, ikiwemo SimBanking, zitawasaidia wajasiriamali kurahisisha malipo na kuboresha usimamizi wa fedha, huku jukwaa hilo likiwa fursa ya kujifunza, kujenga mahusiano na kupanua masoko ya biashara zao.