Habari
NAIBU WAZIRI LONDO AAHIDI KUFUATILIA CHANGAMOTO ZA VIWANDA KUKUZA UZALISHAJI WA NDANI
📌 Asisitiza umuhimu wa kuboresha miundombinu na kuhakikisha leseni za viwanda zinaendana na shughuli halisi za uzalishaji;
📌 Serikali kuendelea kuhamasisha ujenzi wa viwanda vipya na kutatua changamoto za viwanda vilivyopo;
📌 Atembelea viwanda vya Insignia limited coral paints na Mara Nile Group Limited vilivyoko mkoa wa Pwani;
📌 Viwanda vya ethanol kuongeza mahitaji ya mahindi na kuchochea uzalishaji wa zao hilo kwa matumizi ya viwandani.
Kibaha, Pwani.
Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb), amefanya ziara katika viwanda vya Insignia limited Coral Paint na Kiwanda cha kuzalisha Ethanol cha Mara Nile vilivyoko Kibaha mkoa wa Pwani, kwa lengo la kujionea shughuli za uzalishaji kwenye Kongani zilizopo mkoa wa Pwani na kusikiliza changamoto na namna ya kuzitatua.
Akiwa kwenye kiwanda cha Insignia sambamba na Mkuu wa wilaya ya Kibaha aliyeambatana nae, Bwana Fadhili Nkurlu pamoja na wadau mbalimbali Mhe. Londo amesema,
Serikali inaendelea kuhamasisha ujenzi wa viwanda vipya pamoja na kutembelea viwanda vilivyopo ili kubaini changamoto zinazokwamisha uzalishaji na kuzitafutia ufumbuzi.
Amesema Mkoa wa Pwani una nafasi muhimu katika kukuza sekta ya viwanda kutokana na fursa zake za uwekezaji na umuhimu wake katika shughuli za kiuchumi na kumpongeza mwekezaji wa kiwanda hicho kupitia Mkurugenzi wake Bwana Isack Kiwango kwa kupanua uwekezaji kwenye uzalishaji wa rangi pamoja na bidhaa za vifungashio.
Kiwanda cha Insignia, ambacho kilianza shughuli zake Temeke kabla ya kuhamia Kibaha, kinajishughulisha na uzalishaji wa rangi pamoja na bidhaa za vifungashio vya plastiki na chuma. Kwa upande wake, mkurugenzi wa kiwanda hicho, Bwana Isack, amesema kiwanda kina matarajio ya kupanua shughuli zake na kutoa ajira zisizopungua 1,000, huku akiomba Serikali kusaidia kutatua changamoto za miundombinu, hususan barabara zinazohudumia maeneo ya viwanda.
Akiwa katika kiwanda cha kutengeneza Ethanol cha Mara Nile, Mhe. Londo amesema kiwanda hicho kinatatarajia kuleta mapinduzi kwenye kilimo kupitia Teknolojia ya kuzalisha ethanol kwa kutumia mahindi na hivyo kuongeza matumizi ya mahindi katika shughuli za viwandani, ikiwemo uzalishaji wa ethanol.
Akitoa majumuisho ya ziara hiyo Mhe Londo amesema pia mahitaji ya mahindi yataongezeka kwasababu ya matumizi ya viwanda na hivyo zao hilo kuongezeka thamani na kusisitiza umuhimu wa kutafuta matumizi na masoko mbalimbali ya mahindi ili kuongeza thamani ya zao hilo na kupanua fursa za kibiashara kwa wakulima.
Akizungumza katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Londo amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha leseni zinazotolewa kwa viwanda zinaendana na shughuli halisi zinazofanyika. Amesema ni muhimu kufuatilia viwanda vinavyopewa leseni za uzalishaji kamili lakini katika utekelezaji wake vinafanya shughuli za kuunganisha bidhaa pekee, ili kuhakikisha shughuli za viwanda zinaendana na madhumuni ya leseni zao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Fadhili Nkurlu, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa sekta binafsi katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na kutatua changamoto zinazokabili wafanyabiashara na wawekezaji.
Ziara hiyo ni sehemu ya maandalizi ya uzinduzi wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya mwaka 2025 na Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati, Toleo la 2025, unaotarajiwa kufanyika Novemba 4, 2026. Sera hizo zinalenga kutoa mwelekeo wa maendeleo ya viwanda na kukuza shughuli za wajasiriamali nchini.
