Habari
KAMATI YA BUNGE YAPONGEZA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA NA TAASISI ZAKE KWA KUTENGENEZA FURSA KWA WANANCHI.
📌 TanTrade na SIDO wawasilisha taarifa za utekelezaji wa majukumu
📌 Juhudi zinazofanywa na Wizara pamoja na Taasisi zake zimeanza kuonyesha matokeo chanya kwa wananchi katika kuimarisha mazingira ya biashara na uanzishaji wa viwanda vidogo sana, vidogo na vyakati.
Dodoma.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeipongeza Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na taasisi zake, Mamlaka ya Maendeleo ya BiasharaTanzania(TanTrade) na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) kwa hatua zinazochukuliwa katika kutekeleza majukumu yao na kuboresha mazingira ya kukuza viwanda vidogo sana, vidogo na viwanda vya kati na biashara nchini.
Pongezi hizo zimetolewa Oktoba 15, 2026 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Deodatus Mwanyika (Mb), wakati wa kikao cha kupokea na kutathmini taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia taasisi zake, kilichofanyika Bungeni jijini Dodoma.
Kamati hiyo imepokea mawasilisho kutoka taasisi mbili za Wizara ya Viwanda na Biashara ambazo TANTRADE na SIDO.
TanTrade imepongezwa kwa kuendelea kutatua changamoto za wafanyabiashara kwa kupitia Kliniki za biashara, taarifa za masoko na biashara (Tanzania Trade Portal) na kupitia Rajamu ya 'Made in Tanzania'.
Aidha, TanTrade imeendelea kuwatafutia wananchi masoko ya bidhaa wanazozalisha na kuwa na bei nzuri za kuwainua kiuchumi.
SIDO imeendelea kuwezesha wananchi kwa kuwahamasisha kuanzisha viwanda vidogo sana ambavyo vinazalisha bidhaa za wajasiriamali kama vile vifungashio, mashine za kuchakata asali, mafuta ya kula, sabuni na mashine za kuongeza thamani katika mnyororo wa uzalishaji. Pia SIDO imepongezwa kwa kuendelea kuongeza kongani za viwanda darasa vya wajasiriamali na wafanyabiashara.
Mhe. Mwanyika amesema juhudi zinazofanywa na Wizara pamoja na Taasisi zake zimeanza kuonyesha matokeo chanya, hususan katika kuimarisha mazingira ya biashara, uzalishaji na uwekezaji nchini.
Aidha, Mhe. Mwanyika ameitaka Wizara ya Viwanda na Biashara kuendelea kuziwezesha taasisi zake katika nyanja zote ili ziendelee kutekeleza majukumu yake kwa weledi ili kuinua uchumi wa viwanda na kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb), amesema Wizara imepokea pongezi hizo pamoja na maelekezo na ushauri uliotolewa na Kamati na kuahidi kuyafanyia kazi kwa lengo la kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi na kuongeza ufanisi katika sekta ya viwanda na biashara.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Balozi Waziri Salum, amesema wizara inaendelea kushirikiana na taasisi zake ili kukuendelea kutatua changamoto zinazowakabili wananchi. Wizara ya Viwanda na Biashara haikwepeki katika maisha ya kila siku.
