Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

TANZANIA YAWAAGA WAFANYABIASHARA 170 WANAOSHIRIKI MAONESHO YA CANTON FAIR NCHINI CHINA


📌Waagwa rasmi na Naibu Katibu Mkuu Viwanda na Biashara Aristides Mbwasi;

📌Waaswa kutumia fursa za biashara nchini China kuinadi Tanzania kukuza biashara na pato la Taifa


*Dar es Salaam.* 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na biashara  Bw. Aristides Mbwasi ,Leo amewaaga Wafanyabiashara 170 kutoka nchini Tanzania wanaotarajia kushiriki maonesho ya kimataifa ya Canton Fair 2026 yatakayofanyika nchini China.

Akizungumza wakati wa kuwaaga wafanyabiashara hao Bw. Mbwasi amewaasa wafanyabiashara hao kutumia fursa ya ziara hiyo nchini China kutafuta masoko mapya, kujifunza teknolojia za kisasa na kujenga ushirikiano wa kibiashara na wadau wa kimataifa, hatua inayolenga kuongeza ushindani wa biashara za Tanzania katika soko la dunia.

Safari hiyo iliyoratibiwa na Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) itafanyika kuanzia tarehe 13 hadi 27 Oktoba 2026, huku washiriki wakisafiri kwa awamu mbili, ambapo kundi la kwanza litaondoka Oktoba 13 na la pili Oktoba 16.

Aidha Mbwasi aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara kufanya shughuli zao ndani na nje ya nchi na kuongeza kuwa upo umuhimu mkubwa kwa wafanyabiashara kutumia fursa zilizopo kupanua masoko yao na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Kwa upande wake, Rais wa TWCC, CPA Mercy Silla, aliwapongeza wanachama kwa kuchukua hatua ya kutafuta fursa za biashara katika masoko ya kimataifa. Alisisitiza umuhimu wa kutumia kikamilifu fursa zinazotolewa na TWCC, akieleza kuwa chemba hiyo ni jukwaa muhimu linalowaunganisha wafanyabiashara na maarifa, mitandao na fursa za kukuza biashara zao.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC, Dkt. Mwajuma Hamza, alisisitiza umuhimu wa washiriki kuzingatia maelekezo ya safari, usalama na maandalizi ya kibiashara ili kuhakikisha safari inafanyika kwa usalama na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kupitia ushiriki katika Canton Fair 2026, wafanyabiashara hao wanatarajiwa kupata fursa ya kujifunza teknolojia za kisasa za uzalishaji, kukutana na wazalishaji na wasambazaji wa kimataifa, kutambua bidhaa zenye mahitaji katika masoko na kujenga mahusiano yatakayoweza kuzaa ushirikiano na mikataba mipya ya kibiashara.

Hatua hiyo inaendeleza juhudi za TWCC za kuwaunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na fursa za kimataifa, kuwawezesha kupanua wigo wa masoko na kuimarisha biashara zao. Maarifa na mitandao watakayopata washiriki yanatarajiwa kusaidia kukuza biashara na kuchangia maendeleo ya sekta ya viwanda na biashara nchini Tanzania.