Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

USHIRIKIANO KATI YA TANZANIA NA URUSI UNAENDELEA KUZAA MATUNDA- LONDO


Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (mb) amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi unaendelea kuzaa matunda makubwa katika sekta za uwekezaji, biashara, utafiti wa kisayansi, afya na maendeleo ya viwanda, kufuatia ziara ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Urusi.

Amesema hayo wakati wa Siku maalum ya Urusi katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) Julai 09,2026 ambapo amesema uwepo wa idadi kubwa ya wafanyabiashara na washiriki kutoka Urusi ni ushahidi kuwa uhusiano kati ya mataifa hayo umeimarika na umeanza kuleta fursa mpya kwa Tanzania.

Ameeleza kuwa kwa miaka mingi Urusi imekuwa mshirika muhimu wa Tanzania katika kujenga rasilimali watu kupitia elimu, ambapo wataalamu wengi wa Kitanzania wakiwemo madaktari na wahandisi wamepata mafunzo nchini humo na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.

Londo amesema matokeo ya ziara ya Rais Samia yanaonekana kupitia ongezeko la wawekezaji na wafanyabiashara wa Urusi wanaoonesha nia ya kuwekeza katika viwanda vya kutengeneza dawa, tafiti za tiba, uzalishaji wa chanjo pamoja na ushirikiano wa kisayansi kati ya taasisi za Tanzania na Urusi.

Aidha, amesema Serikali ya Urusi imeonesha utayari wa kushirikiana na Tanzania katika tafiti za anga ya juu na maendeleo ya teknolojia ya satelaiti, sayansi na teknolojia na kuiwezesha Tanzania kuongeza uwezo wa uzalishaji na kukuza ushindani wa bidhaa zake katika soko la dunia na kufikia malengo ya uchumi wa kisasa .

Londo amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kutekeleza maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji ili Watanzania wanufaike na fursa zinazotokana na ushirikiano wa kimataifa pamoja na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuongeza thamani ya mazao na bidhaa za Tanzania, kujenga uchumi wa viwanda wenye ushindani wa kimataifa .

Kwa Upande wake Balozi wa Urusi Nchini Tanzania Mhe.Andrey Avetisyan amesema ni furaha kuwa sabasaba Katika kuunganisha Biashara baina na nhi hizo mbili na Kampuni za urusi zimekuja Nchini kutafuta Masoko na ushirikiano wa kibiashara