Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

LONDO ASISITIZA NIDHAMU NA UTENDAJI WA MFANO KWA WATUMISHI


Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb), ametoa rai kwa Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara hiyo kuwa kioo cha utendaji kwa kufanya kazi kwa kujituma, weledi, na uadilifu ili kuleta tija na kuwa mfano wa kuigwa na Watumishi wengine.

Amewasisitiza Watumishi hao kuwa nidhamu ya kazi ndiyo itakayohakikisha ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku na kutimiza malengo ya Wizara na Taifa kwa ujumla.

Ameyasema hayo Mei 04, 2026 wakati akifungua Kikao cha Baraza hilo katika Ofisi za Wizara, Mtumba Jijini Dodoma, na kubainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Mheshimiwa. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanya maboresho makubwa ya mazingira ya kazi na maslahi ya Watumishi hivyo hawana budi kufanya kazi kwa bidii.

Aidha, amesema Wajumbe hao wamebeba maono na matarajio ya watumishi wa Wizara, hivyo wanapaswa kuibua masuala ya kisera yatakayochochea uendelezaji wa sekta ya viwanda na biashara nchini.

Vilevile, amewataka Wajumbe kutumia hekima na busara katika kugawa rasilimali chache zilizopo ili ziweze kutatua kero za msingi kwa uwazi, hatua itakayosaidia kuepuka migongano wakati wa utekelezaji wa Bajeti na kuhakikisha kuwa vipaumbele vilivyowekwa vinaleta tija na ustawi wa kudumu kwa Watanzania katika sekta ya viwanda na biashara.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Waziri Salum, ameziagiza Idara na Vitengo vya Wizara kuhakikisha kunakuwepo na usimamizi madhubuti wa Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo ili ziweze kutoa matokeo chanya yanayotarajiwa na Wananchi.

Amesisitiza kuwa ufuatiliaji wa karibu na utendaji wa kimkakati ndani ya Taasisi hizo ndio utakaowezesha sekta ya viwanda na biashara kuwa na mchango unaoonekana katika kukuza uchumi na kutatua kero za Wananchi.