Habari
Dkt. Kijaji aitaka Bodi ya WMA kuwalinda walaji

Dkt. Kijaji aitaka Bodi ya WMA kuwalinda walaji
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ameisistiza Bodi mpya ya Ushauri ya Wakala wa Vipimo kuhakikisha walaji wanalindwa kupitia uhakiki wa vipimo ili wanaponunua bidhaa mbalimbali wapate kuona thamani ya fedha katika bidhaa hizo.
Waziri Kijaji ameyasema hayo alipokuwa akizindua Bodi ya Sita ya Wakala wa Vipimo uliofanyika Julai 27, 2023 jijini Dodoma.
Aidha, Ameitaka Bodi hiyo kufanya kazi yake kwa weledi na kuhakikisha inasimamia usalama wa mali za watanzania kupitia vipimo sahihi ili kufikia matarajio ya Serikali katika kitekeleza vipaumbele vya Serikali kwenye usimamizi wa matumizi sahihi ya vipimo nchini ili kuwahudumia wafanyabiashara na wawekezaji kuwalinda Walaji.
Dkt. Kijaji pia ameielekeza Bodi hiyo
kuhakikisha inatokomeza suala la lumbesa ambalo limekuwa likilalamikiwa katika maeneo mengi ili kurudisha matumaini ya wakulima nchini.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Vipimo, Dkt. Eliza Alfred Mwakasangula amemshukuru Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), pamoja na Menejimenti ya Wakala kwa kuahidi kusimamia na kufanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa na kushauri Wizara ipasavyo kwenye masuala ya vipimo ili kuhakikisha wakala inaendelea kutoa huduma bora kwa Wananchi inao wahudumia.
Kwa upande wa Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo Bi. Stella Kahwa amemshukuru Waziri kwa kuteua Bodi ambayo itasaidia kuleta maendeleo kwa wakala, ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya vipimo vinavyohakikiwa kwa mwaka na kuhakikisha Wakala inaendelea kuchangia katika mfuko mkuu wa Serikali ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi