Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Dkt. Philip Mpango aielekeza Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kusimamia uondoaji wa  vikwazo vinavyokwamisha biashara ya Tanzania  katika nchi za EAC, SADC na AfCFTA.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ameielekeza Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kusimamia uondoaji wa 
 vikwazo vinavyokwamisha biashara ya Tanzania  katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ( SADC), Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) ili kurahisisha ufanyaji biashara baina ya nchi hizo.

Dkt. Mpango ameyasema hayo wakati akifunga rasmi Maonesho ya  46 ya Kimataifa ya kibiashara yaliyoanza tarehe 28 Juni hadi 13 Julai 2022 jijini  Dar es salaam ambapo  alitembelea baadhi ya mabanda ya  Taasisi na Wafanyabiashara ili kujionea bidhaa na Teknolojia zinazotumika katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.

Makamu wa Rais pia amezielekeza Taasisi za Masoko za Zanzibar na Bara kushirikiana na Wizara ya Mambo ya  Nje na Ushieikiano wa Afrika Mashariki kushughulikia changamoto za masoko na vifungashio vyenye ubora vya bidhaa za Tanzania, upatikanaji wa malighafi za baadhi ya bidhaa ikiwemo bidhaa za mafuta ya kula.

Vilevile,  amezitaka taasisi za utafiti kufanya kazi za ziada ya kutafiti mbegu bora za mafuta ya kula zenye kutoa mafuta mengi zaidi.

Dkt. Mpango pia ameyataka Makampuni ya simu kushirikiana na Taasisi kuwekeza katika teknolojia za kidijitali zaidi.

Aidha, ameitaka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara kufanya tathimini ya maonesho ya Sabasaba ili kuboresha maonesho yajayo na  ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kukaa na sekta ya fedha kuangalia namna watu wanavyoweza kupata mtaji kwa ajili ya biashara na uwekezaji.

Dkt. Mpango amewasisitiza Wafanyabiashara Kuzingatia kanuni za ushindani kwa kuheshimu mikataba na kuwataka waongeze uzalishaji kwenye bidhaa zenye mahitaji makubwa nchini kama sukari, mafuta ya kula na vifaa vya ujenzi ili nchi iweze kujitosheleza.