Habari
DKT. WAPONGEZA WAFANYAKAZI WA NDC

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, amewapongeza wafanyakazi wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kwa bidii na mshikamano waliouonyesha katika utekelezaji wa majukumu yao, akiwataka waendelee kuzingatia miongozo na maadili ya Utumishi wa Umma.
Akizungumza Agosti 29, 2025 katika kikao kazi kilichohudhuriwa na Menejimenti na watumishi wa NDC, pamoja na Mkurugenzi Mwendeshaji wa shirika hilo, Dkt. Nicolaus Shombe, Dkt. Abdallah amesema kikao hicho ni fursa muhimu ya kushirikiana mawazo, kubadilishana uzoefu na kujadili mustakabali wa Shirika katika mchango wake kwa Maendeleo ya Taifa.
“Ni fahari kubwa kwangu kuona ari, juhudi na bidii mnazionyesha kila siku katika kazi zenu, ambazo zinachangia moja kwa moja kufanikisha malengo ya shirika letu,” alisema Dkt. Abdallah.
Katika hotuba yake, Katibu Mkuu alisisitiza juu ya umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii na kujituma, kuzingatia maadili ya kazi, na kuonesha uzalendo kwa Shirika na Taifa. Pia alihimiza watumishi kushughulikia changamoto kwa njia sahihi na kushirikiana kwa dhati na kwa upendo miongoni mwao ili kufanikisha malengo ya pamoja.
Katibu Mkuu aliambatana pia na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Suleiman Selela, ambaye naye ameipongeza Menejimenti ya NDC kwa mshikamano wao katika kusimamia shughuli za Shirika.
Kwa upande wake, Dkt. Nicolaus Shombe, Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, alieleza kuwa kupitia kiwanda mama cha TBPL, shirika lipo mbioni kuanza uzalishaji wa mbolea ya viuatilifu, huku shughuli katika Kiwanda cha KMTC kilichopo Moshi, mkoani Kilimanjaro zikiendelea vyema.
Aidha, Dkt. Shombe alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna alivyofanikisha ulipaji wa fidia kwa miradi wa Liganga na Mchuchuma pamoja na mradi wa Magadi soda, hatua muhimu inayowezesha utekelezaji wa mradi hiyo mikubwa ya kimkakati ya serikali.