Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

KAPINGA: MKUMBI II KUWEZESHA UKUAJI WA PATO LA TAIFA KWA ZAIDI YA ASILIMIA 20


Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), amesisitiza umuhimu wa Mkumbi II wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji katika kufanikisha malengo makubwa ya Taifa, akionesha kuwa mafanikio ya Mkumbi I yametengeneza msingi thabiti wa Maendeleo ya Uchumi na Viwanda nchini.

Akizungumza katika mkutano wa uhakiki wa rasimu ya Mkumbi II uliofanyika katika Ukumbi wa Hazina Machi 11, 2026 jijini Dodoma.

Mkutano huo umewakutanisha Wakuu wa mikoa na wilaya, Makatibu Tawala, pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri, kwa lengo la kutoa maoni na kuhakikisha utekelezaji wa mpango huo unafanyika kwa ufanisi.

Kapinga amebainisha kuwa Mkumbi II itahakikisha malengo ya ukuaji wa uchumi yanafanikiwa, pia mkakati huu unalenga kuona pato la Taifa likikua kwa zaidi ya asilimia 20 ndani ya miaka 25 ijayo, huku Viwanda vipya zaidi ya elfu 10 vikitarajiwa kuanzishwa kupitia mkakati wa Maendeleo ya Viwanda wa miaka sita.

Aidha, Waziri Kapinga amesisitiza kwamba ushirikiano wa karibu kati ya Wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na Makatibu Tawala ni muhimu ili kuhakikisha utekelezaji unafanyika kwa mtazamo mmoja. “Ni mategemeo makubwa sana, hivyo viongozi wote wanapaswa kushirikiana na kuwa na sura moja katika utekelezaji wa mpango huu."

Mkutano huo ni hatua ya muhimu katika kuhakikisha kuwa Sera na Mikakati ya Biashara na Ywekezaji zinakidhi malengo ya muda mrefu ya Dira ya Taifa 2025.