Habari
DKT.SERERA: MFUMO WA STAKABADHI GHALANI WAONGEZA USHINDANI WA SOKO LA MAZAO
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Serera, ametoa wito kwa wadau wa kilimo na biashara kuendelea kutumia Mfumo wa Stakabadhi ghalani ambao umeleta ushindani katika soko la bidhaa za kilimo na kuwawezesha wakulima kupata faida kubwa kutokana na bei nzuri za mazao yao.
Vilevile ameipongeza Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) kwa kusimamia vyema Mfumo wa stakabadhi ghalani unaotekelezwa katika Halmashauri ya Karatu, mkoani Arusha ambao umeleta tija kubwa kwa wakulima na wafanyabiashara wa mazao.
Hayo ameyasema Oktoba 22, 2025 baada ya kutembelea maghala ya Karatu Gilole, Rhotia na Union service Store( NMC ) yanayotumia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa lengo la kujionea shughuli za Uzalishaji, kisikiliza na kutatua changamoto zilizopo
Aidha, amesema Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo imejipanga kuhakikisha bidhaa zote zinazofika kwa mlaji zinakuwa salama na zenye ubora unaozingatia viwango vya usalama wa chakula, ili kupunguza magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanayotokana na matumizi ya vyakula visivyo salama.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala, Bw. Asangye Bangu amesema Mfumo huo umepokelewa vizuri na wakulima wa mbaazi wilayani Karatu, na kwamba umechangia kupatikana kwa bei nzuri ya zao hilo sokoni.
“Tunawahakikishia wanunuzi na watumiaji kwamba bidhaa zinazotolewa kupitia Mfumo huu zina ubora unaoendana na thamani ya fedha zao. Mfumo huu unaleta uwazi, usawa na faida kwa pande zote,” amesisitiza.
Awali Mkusanya mali Bi Gladness Tarimo, amesema mfumo wa stakabadhi ghalani umeleta manufaa makubwa kwa vijana kwani umewapa nafasi ya kuuza bidhaa zao kwa bei shindani na inayojulikana wazi katika soko.
Naye, Evarist Silayo, Mfanyabiashara wa mazao ambaye kampuni yake inamiliki maghala katika maeneo matatu nchini ikiwemo Karatu, amesema mfumo huo umeondoa upunjaji na kuongeza uaminifu kati ya wakulima na wanunuzi.
