Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

UANZISHAJI WA KIWANDA KIPYA CHA SBC KUCHOCHEA AJIRA KWA VIJANA DAR NA DODOMA


Kampuni ya SBC Tanzania Ltd, wazalishaji wa vinywaji baridi vya Pepsi, inatekeleza mpango mkubwa kuanzisha kiwanda kipya cha kutengeneza vifungashio vya plastiki jijini Dar es Salaam na inatarajia kufungua tawi jipya la kiwanda mkoani Dodoma, miradi inayotarajiwa kuongeza ajira kwa vijana nchini.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), Aprili 2, 2026, alipotembelea Kiwanda hicho jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujionea shughuli za uzalishaji na maendeleo ya uanzishaji wa kiwanda hicho kipya.

Akiwa ameambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Aristides Mbwasi, Waziri Kapinga ameeleza kuwa uanzishaji wa kiwanda cha kutengeneza vifungashio vya plastiki hapa nchini ni hatua muhimu itakayopunguza utegemezi wa kuagiza malighafi hiyo kutoka nje, kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza ajira uongezaji wa ajira kwa vijana wengi wa Kitanzania katika kiwanda cha Dar es Salaam na tawi jipya la Dodoma.

Aidha, Waziri Kapinga amesisitiza kuwa Wizara yake itahakikisha inasimamia Sera zinazochochea ukuaji wa viwanda mama ili kuimarisha mnyororo wa thamani na kusaidia teknolojia zinazozalisha bidhaa bora kwa soko la ndani na nje.

Waziri Kapinga amebainisha kuwa ameridhishwa na kasi ya maendeleo ya mradi huo wa SBC na amesema kuwa ujenzi wa tawi la Dodoma utasaidia kusogeza bidhaa karibu na walaji na kuimarisha uchumi wa makao makuu.

Aidha ametoa wito kwa wawekezaji wengine kufuata nyayo za SBC kwa kuanzisha viwanda vinavyoongeza thamani ya malighafi hapa nchini ili kukuza uchumi wa taifa.

Naye, Mkurugenzi wa Mahusiano wa kampuni ya SBC (Pepsi), Bw. Foti Nyirenda, amesema kuwa hatua hizo za upanuzi wa kiwanda cha Dar es Salaam na ufunguzi wa tawi jipya la Dodoma zitafungua fursa nyingi za ajira kwa Watanzania na utaongeza ufanisi wa uzalishaji na usambazaji wa bidhaa nchi nzima.