Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SERIKALI YAJIDHATITI KUONGEZA UJUZI KUFANIKISHA AJENDA YA UCHUMI WA VIWANDA


Serikali imejidhatiti kuhakikisha nchi inazalisha rasilimali watu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji halisi ya soko la ajira ili kufanikisha Ajenda ya Uchumi wa Viwanda.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo(Mb) Februari 9, 2026 jijini Dar es Salaam katika Uzinduzi wa Mpango wa Pamoja wa Ushirikiano kati ya Vyuo na Viwanda.

Mheshimiwa Londo amesema sekta ya Viwanda na Biashara ni mhimili muhimu wa uchumi wa Taifa kutokana na mchango wake katika kukuza Pato la Taifa, kuzalisha ajira, kuongeza thamani ya malighafi za ndani na kupanua biashara ya ndani na nje ya nchi.

Sekta ya viwanda inachangia kati ya asilimia nane hadi tisa ya pato la Taifa huku sekta ya Biashara na Usambazaji ikichangia zaidi ya asilimia 10.

Hatahivyo pamoja na mafanikio yaliyopatikana, bado kuna pengo kubwa kati ya ujuzi unaotolewa na Taasisi za Elimu na ujuzi unaohitajika na waajiri, hali inayosababisha changamoto katika upatikanaji wa ajira kwa wahitimu wengi.

Waajiri wanahitaji wahitimu wenye ujuzi wa vitendo, ubunifu, uelewa wa teknolojia za kisasa pamoja na maadili ya kazi yanayokidhi ushindani wa kimataifa.

Aidha, mpango huo wa pamoja utaimarisha mitaala ya Elimu ili iendane na mahitaji ya sekta za vipaumbele ikiwemo viwanda vya uzalishaji, uongezaji thamani wa mazao ya kilimo, nguo na ngozi, madini, ujenzi, biashara ya kimataifa na TEHAMA.

Pia waajiri watashiriki kikamilifu katika uundaji wa mitaala na utoaji wa mafunzo kwa vitendo ili wahitimu wawe tayari kuajiriwa au kujiajiri mara baada ya kumaliza masomo yao.

Mafanikio ya mpango huo yatategemea ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na Sekta Binafsi, pamoja na ushiriki wa vijana na wanawake katika shughuli za uzalishaji.

Mpango huo ni nyenzo muhimu ya kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuifanya Tanzania kuwa Taifa la kipato cha juu lenye uchumi shindani unaoongozwa na Viwanda, Biashara na rasilimali watu yenye ujuzi na ubunifu.