Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SERIKALI YASISITIZA USHIRIKIANO KUTOKOMEZA POMBE HARAMU NCHINI


Serikali imesisitiza umuhimu wa ushirikiano baina yake, sekta binafsi, na wadau mbalimbali katika kudhibiti uzalishaji na uuzaji wa pombe zisizokidhi vigezo, ikibainisha kuwa nguvu ya upande mmoja pekee haitoshi kushinda vita hiyo.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb), wakati wa uzinduzi wa matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi ya Euro Monitor Februari 5, 2026 jijini Dar es Salaam.

Londo amebainisha kuwa bila ushiriki wa karibu wa wadau wa sekta binafsi, itakuwa vigumu kutokomeza pombe haramu ambazo zimekuwa mwiba katika kulinda ushindani wa kibiashara, mapato ya serikali, na zaidi, afya za walaji.

"Serikali pekee bila ushiriki wa sekta binafsi na wadau wengine haitaweza kufikia malengo ya kutokomeza pombe haramu. Ushirikiano huu ni muhimu ili kulinda ushindani wa haki sokoni na kuhakikisha usalama wa afya za wananchi wetu," alisema Londo.

Utafiti huo wa Euro Monitor umeanika aina kuu za pombe haramu zinazosumbua soko, ambazo ni Pombe zinazoingizwa nchini kwa njia za magendo, Pombe zinazozalishwa ndani ya nchi kinyume na taratibu na sheria zilizowekwa , Pombe za kienyeji ambazo hazikidhi viwango vya ubora na usalama kwa binadamu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Viwanda nchini (CTI), Bw. Leodegar Tenga, amesema kuwa biashara hiyo haramu inarudisha nyuma ukuaji wa sekta ya viwanda.