Habari
SERIKALI IPO TAYARI KUWASIKILIZA WAWEKEZAJI - BALOZI SALUM
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Wizara nyingine ipo tayari kuendelea kuwasikiliza na kuwasaidia wawekezaji nchini katika kuondoa changamoto zao mbalimbali.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda Mhe.Balozi Waziri Salum wakati akihitimisha ziara yake ya kwanza Mkoani Tanga ikiwa ni muendelezo wa kukagua na kuona ufufuaji wa Viwanda Mkoani humo ili kutimiza dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutaka kurejeshwa kwa Tanga ya Viwanda ili kuchagiza upatikanaji wa ajira kwa wingi kwa vijana wa Mkoa huo., Aprili 25,2026.
Balozi Salum amesema Wizara ya Viwamda na Biashara inafikika kirahisi na ipo tayari muda wowote kuwafikia wawekezaji wote wenye changamoto ili kutatua changamoto zao kwani ni imani yake kama Serikali hakuna changamoto ya mwekezaji ambayo Serikali itashindwa kuitatua.
Aidha amesema Serikali ya awamu ya sita inahitaji wawekezaji wake kukua zaidi hivyo inaendelea kuweka mazingira rafiki ya kuvutia wawekezaji na kuwalea wale ambao wamewekeza nchini.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Tanga Bw.Rashid Mchata amesema uwepo wa ziara hiyo katika Mkoa huo ni nia ya dhati ya Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara ya kufufua Viwanda Mkoa wa Tanga ambapo itasaidia upatikanaji wa ajira kwa vijana wengi zaidi kwani baadhi ya viwanda vimeanza kazi.
