Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

TBPL YAAHIDI KUONGEZA UWEKEZAJI NA UBUNIFU BAADA YA KUSAINI MAKUBALIANO NA TAASISI ZA UTAFITI


Mkurugenzi na Mwenyekiti wa Bodi ya TBPL amesema kampuni hiyo itaendelea kuwekeza katika ubunifu, matumizi ya teknolojia za kisasa na kuzingatia viwango vya ubora ili kuongeza uwezo wa uzalishaji, kuchangia ukuaji wa uchumi, upatikanaji wa ajira na maendeleo ya sekta ya afya nchini.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya TBPL na taasisi mbalimbali za utafiti, amesema serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji na ukuaji wa viwanda nchini.

Amesema ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za utafiti na sekta binafsi ni muhimu katika kuhakikisha viwanda vinazalisha bidhaa bora, salama na zenye ushindani ndani na nje ya nchi. Alitaja taasisi mbalimbali ikiwemo TARI kuwa miongoni mwa wadau wanaochangia mafanikio ya sekta hiyo.

Aidha, ameishukuru Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Afya, Wizara ya Kilimo pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI kwa ushirikiano wanaouendelea kuutoa katika kuimarisha maendeleo ya viwanda na sekta nyingine muhimu za uchumi.

Katika hatua nyingine, amesema TBPL imepitia changamoto mbalimbali za kifedha na kiutendaji katika miaka iliyopita, ikiwemo madai ya mishahara ya wataalamu, lakini akapongeza uvumilivu wa wafanyakazi walioendelea kufanya kazi huku wakiamini serikali itatatua changamoto hizo.

Amesema tangu mwaka 2022 Serikali imeendelea kutoa fedha kupitia sekta ya afya ambazo zimechangia kuimarisha utendaji wa Kiwanda hicho na kuwezesha maendeleo ya teknolojia mpya zinazosaidia kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya kilimo.