Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SERIKALI KUENDELEA KUONGEZA AJIRA KUPITIA VIWANDA


Serikali imesema inaendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kurejesha viwanda vilivyosimama uzalishaji nchini, ikiwemo Mkoa wa Morogoro, kupitia tathmini, ufuatiliaji, na kuwatafuta wawekezaji wapya wenye uwezo ili kurejesha uzalishaji na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dennis Londo (Mb), Septemba 02, 2026 Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu Swali Namba 92 la Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro, Mhe. Devotha Mathew Minja, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kurejesha viwanda vilivyosimama uzalishaji Mkoani humo ili kutoa ajira kwa wananchi.

Akijibu swali hilo, Londo ameeleza kuwa kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, viwanda vyote vilivyoshindwa kuendelezwa na wawekezaji wa awali vinaendelea kupatiwa wawekezaji au taasisi zenye uwezo wa kuviendesha upya.

Akitolea mfano wa hatua hizo, amebainisha kuwa Kiwanda cha Mang’ula Mechanical & Machine Tools kilichopo Wilayani Kilombero Mkoani Morogoro tayari kimekabidhiwa kwa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kwa ajili ya kuendelezwa.

Aidha, amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili kuwavutia wawekezaji wengi zaidi kuwekeza kwenye viwanda vipya pamoja na kufufua vilivyosimama uzalishaji.