Habari
SERIKALI YAHIMIZA WAZALISHAJI KUTUMIA TAASISI ZA SERIKALI ILI KUSHINDANA KIMAITAIFA
Serikali imetoa wito kwa wazalishaji na wafanyabiashara nchini kutumia huduma zinazotolewa na taasisi za Serikali katika masuala ya viwango, vipimo, usalama wa bidhaa, usajili na urasimishaji wa biashara ili ziweze kushindana kimataifa kwani Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais wake Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Sekta Binafsi ili kuzalisha, kuwekeza na kupanua masoko ndani na nje ya nchi.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dennis Londo(Mb) wakati akimuakilisha Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Judith Kapinga (Mb) katika Ufunguzi wa Maonesho
ya 21 ya Biashara ya Afrika Mashariki Septemba 03,2026, Jijini Mwanza.
Ameeleza kuwa jukumu la Serikali si kufanya biashara, bali ni kuondoa vikwazo visivyo vya lazima, kuboresha miundombinu na kurahisisha taratibu ili sekta binafsi iweze kukua na kuongeza tija na kusisitiza kuwa ubora si gharama bali ni tiketi kuu inayowezesha bidhaa za Tanzania kupata fursa na kushindana kikamilifu katika masoko ya Afrika na kimataifa.
Aidha Mhe. Londo amezitaka taasisi za Serikali na vyombo vya udhibiti kuwa wawezeshaji badala ya kuwa kikwazo kwa wafanyabiashara, hasa wadogo na wa kati (SMEs). Ameeleza kuwa udhibiti unapaswa kwenda sambamba na utoaji wa elimu, ushauri na huduma kwa wakati ili kusaidia biashara kufuata sheria na kujiimarisha katika mnyororo wa thamani.
Halikadhalika, amewasihi waonyeshaji na wajasiriamali kutochukulia maonyesho ya biashara kama fursa ya kuuza bidhaa kwa siku chache pekee, bali kuyatumia kama jukwaa la kujenga mitandao ya kibiashara, kupata wanunuzi wakubwa, na kusaini mikataba ya usambazaji. Pia amewahimiza wananchi kuunga mkono juhudi hizo kwa kununua bidhaa zilizozalishwa nchini zenye viwango na ubora unaokubalika.
Akiangazia fursa za kijiografia kwa Mkoa wa Mwanza na Kanda ya Ziwa, Mhe. Londo amewahimiza wafanyabiashara kutolenga soko la ndani pekee bali kutumia fursa za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na AfCFTA.
