Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SERIKALI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI KUBORESHA USAFIRISHAJI WA MAKONTENA NA BIASHARA YA KIKANDA


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Serera, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kutatua changamoto za usafirishaji shehena la bidhaa na kuongeza tija kwenye Biashara ya makontena, ili Tanzania inufaike ipasavyo na fursa zilizopo katika masoko ya kikanda kama Ukanda Huru wa Biashara Afrika (AfCFTA), SADC, na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Dkt. Serera ameyasema hayo Oktoba 21, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Baraza la wasafirishaji shehena Tanzania (Tanzania Shippers Council).
Aidha, Wizara inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji na wadau wa usafirishaji ili kuhakikisha mifumo ya biashara inakuwa na ufanisi, ushindani na tija kwa Taifa.

“Sisi kama serikali tunaandaa sera, kanuni na sheria, lakini wanaozitekeleza ni wenzetu wa sekta binafsi. Wao ndio walioko kwenye uwanja wa kazi, wanaona fursa na changamoto. Tunapokutana nao katika mikutano kama hii, tunapata nafasi ya kujadili namna bora ya kuzitumia fursa hizo na kukabili changamoto,” alisema Dk. Serera.

Amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa sekta binafsi katika kukuza uchumi wa nchi, kuongeza ajira na mapato kupitia kodi na tozo mbalimbali, na kwamba mafanikio hayo hayawezi kupatikana bila uwepo wa miundombinu madhubuti ya usafirishaji.

“Tumeshuhudia maendeleo makubwa kama ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), lakini bado tunatakiwa kuhakikisha kuwa miundombinu hii inawafikia wadau wote ili kuongeza ufanisi wa biashara na kurahisisha mnyororo wa thamani,” aliongeza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa baraza hilo, Bw. Clement Kamindu alisema Serikali imeonesha utayari mkubwa wa kushirikiana na wadau kutatua changamoto hizo, ambapo alimtaja Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Serera, kuwa ameahidi ushirikiano wa hali ya juu kwa baraza hilo.

Akizungumzia hali ya sasa ya bandari ya Dar es Salaam, Kamendu alisema kumekuwa na maboresho makubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma, jambo lililosaidia kupunguza ucheleweshaji wa mizigo (foleni).