Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SERIKALI KUENDELEA KUWEKA MAZINGIRA RAFIKI KWA WAZALISHAJI WA MAFUTA YA KULA-LONDO


Serikali imesema itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wazalishaji wa mafuta ya kula ili kukuza uchumi na kuboresha soko kwa wakulima pamoja na wazalishaji wa bidhaa za mafuta nchini kwa kusisitiza kushirikiana na wadau mbalimbali kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto ya malighafi nchini akiongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2020–2050 na mkakati wa kujenga uchumi unaojitegemea.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb), wakati wa Ziara yake katika Kiwanda cha Mafuta cha MAINLAND kilichopo Dodoma, Agosti 31,2026.

Londo amewataka wadau wa sekta hiyo kuongeza ujuzi wa uzalishaji kwa vijana wanaochipukia ili kujenga msingi imara wa uzalishaji kwa miaka ijayo na kuifanya Tanzania isiwe tegemezi wa rasilimali watu kutoka nje, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia na mashine za kisasa zilizopo viwandani kuongeza tija, ubora na ushindani wa bidhaa za ndani katika soko la Tanzania na kimataifa.

Aidha amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uzalishaji wa mafuta ya kula nchini, hususan kwa kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa malighafi inapata suluhisho la kudumu.

Vilevile amekitaja kiwanda hicho kuwa miongoni mwa viwanda vya kimkakati katika uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa ajira, akibainisha kuwa uwekezaji huo unaendana na mkakati wa Taifa wa kujitosheleza kwa mafuta ya kula na kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa na wakulima nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Kiwanda hicho, Bi. Betty Mkwasa, amesema kiwanda hicho kilianza uzalishaji mwaka 2023, huku makao makuu yake yakiwa Dar es Salaam, na kina uwezo wa kuzalisha tani 90,000 za mafuta kwa mwaka, sawa na wastani wa tani 50 kwa siku. Hata hivyo, amesema katika kuongeza upatikanaji wa malighafi ameeleza kuwa mpango uliopo ni kuingia mikataba ya uzalishaji wa malighafi kupitia vyama vya ushirika, ili kuwawezesha wakulima kuwa sehemu ya mnyororo wa uhakika wa upatikanaji wa malighafi kwa kiwanda.