Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SERIKALI ITAENDELEA KULINDA VIWANDA VYA NDANI


Serikali itaendelea. kulinda viwanda vya ndani ikiwemo viwanda vinavyozalisha mabati na soko la ndani kwa kuweka kodi kwa mabati yanayoingizwa kutoka nje na kuweka kodi ya maendeleo ya viwanda.

Vilevile, Wizara ya Viwanda na Biashara itaendelea kutekeleza maono ya Serikali ya Awamu Sita ya ya kukuza Uchumi wa Viwanda kwa kushirikiana na Sekta nyingine na kuchukua hatua zote kuhakikisha maono hayo yanatekelezeka.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga (Mb), wakati wa uzinduzi wa Kiwanda cha Lodhia Industries Ltd uliofanywa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani Februari 12, 2026.

Akimkaribisha Mgeni Rasmi katika Ufunguzi huo , Waziri.Kapinga amefafanua kuwa Lodhia ni mojawapo ya Kiwanda kati ya viwanda vitano vikubwa vinavyozalisha mabati nchini ambavyo vinachangia Tanzania kuzalisha mabati tani 900,000 kwa mwaka na matumizi ya ndani ni tani 430,000 na kuwa na ziada inayouzwa nje ya nchi hivyo uwepo wa Kiwanda cha Lodhia katika soko unatoa uhakika wa Soko la ndani na nje.

Aidha, Waziri Kapinga amebainisha kuwa katika kuhakikisha udhibiti wa soko na kuhakikisha bidhaa zenye ubora zinaingia sokoni Shirika la Viwango Tanzania (TBS), na Tume ya Ushindani (FCC), zimekuwa zinatumika kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa bora za mabati ambapo katika kipindi cha Julai – Desemba 2025. Mabati – 776,800 yasiyo na ubora yamezuiwa.