Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SERIKALI KUBORESHA BIASHARA YA SENENE, KUUZWA MIJI MIKUBWA


Serikali inaendelea kutafuta na kufungua masoko ya uhakika kwa bidhaa za senene ili kuwaunganisha wafanyabiashara na miji mikubwa na kuboresha biashara hiyo ili kuinua uchumi wa wananchi wanaotegemea biashara hiyo Bukoba, mkoani Kagera.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb), Januari 31, 2026 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Bukoba Mjini, Mhe. Mhandisi Johnston Mutasigwa.

Katika swali lake, Mbunge huyo amehoji, Serikali ina mpango gani kuwapatia wauza senene masoko na vifaa bora vya kutegea senene.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri amesema hii inajumuisha kuwaunganisha wafanyabiashara wa senene na masoko ya miji mikubwa nchini.

Pia, kuwashirikisha katika maonesho ya biashara ya kitaifa na kikanda na kutangaza senene kama bidhaa ya kipekee ya Kanda ya Ziwa yenye uwezo wa kuingia kwenye masoko mapana ya Afrika Mashariki na kwingineko.

Amesema Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), kwa kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) pamoja na VETA imeendelea kufanya tafiti mbalimbali zinazolenga kuendeleza na kuboresha biashara ya senene katika Mkoa wa Kagera.

Katika swali la nyongeza, Mbunge huyo amehoji Serikali ina mpango gani kuwatengea eneo wafanyabiashara wa senene ili kuuza bidhaa zao kwa uhakika.

Akijibu swali hilo, Londo amesema Serikali kupitia halmashauri ya Manispaa ya Bukoba wameendeleza ujenzi wa soko la senene lengo likiwa kuwaweka wafanyabiashara pamoja.