Habari
SERIKALI YAITAKA SEKTA YA VIWANDA KUONGEZA UZALISHAJI, MATUMIZI YA TEKNOLOJIA
Serikali imeitaka sekta ya Viwanda kuongeza uzalishaji, kuwekeza katika teknolojia na kutafuta masoko mapya, katika wakati ambao inaendelea kushughulikia changamoto zinazokwamisha uzalishaji wa sekta hiyo.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb), Septemba 1, 2026, alipotembelea Kiwanda cha Mvinyo cha Alko Vintages Co. Ltd jijini Dodoma kujionea shughuli za uzalishaji, mafanikio na changamoto zinazokikabili Kiwanda hicho kinachotumia zao la Zabibu kama Malighafi.
Akizungumza katika Ziara hiyo amesema uwekezaji katika usindikaji wa zabibu una nafasi muhimu katika kuongeza thamani ya zao hilo, kuwapatia wakulima soko na kuchochea ajira huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano kati ya viwanda na wakulima ili kuhakikisha upatikanaji wa malighafi bora na za kutosha.
Londo amesema Wizara imepokea changamoto zinazohusu upatikanaji wa malighafi, gharama za uzalishaji, vifaa na masoko na kwamba zitafanyiwa kazi kwa kushirikiana na taasisi husika.
Aidha, ameipongeza Alko Vintages kwa mchango wake katika kuongeza thamani ya zabibu na kukuza tasnia ya mvinyo nchini, akieleza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuongeza uzalishaji, ajira na ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Vilevile, Londo ametoa wito kwa taasisi za Serikali, sekta binafsi na wananchi kuendelea kuunga mkono bidhaa zinazozalishwa nchini, ili bidhaa za Tanzania ziweze kushindana katika masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.
