Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Mb) amezitaka Halmashauri nchini kuwawezesha Maafisa Biashara kushiriki kikamilifu katika mikutano na Mafunzo


Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Mb) amezitaka Halmashauri nchini kuwawezesha Maafisa Biashara kushiriki kikamilifu katika mikutano na Mafunzo mbalimbali kwa lengo la kubadilishana uzoefu, fursa na kupanga mikakati mbalimbali ya kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kujenga Uchumi wa Taifa.

Amebainisha hayo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Nne wa Chama cha Maafisa Biashara Wanawake Tanzania (TAWTO) ambao umehudhuriwa na Maafisa Biashara Wanawake kutoka Mikoa mbalimbali nchini leo Agosti 20, 2025 Jijini Tanga.

Dkt.Jafo amesema Maafisa Biashara hao wamekuwa nguzo muhimu katika kusaidia upatikanaji wa mapato katika Halmashauri nyingi hivyo ni muhimu changamoto zao kutatuliwa ikiwemo vitendea kazi na stahiki zao.

Katika hatua nyingine Dkt. Jafo amesema atahakikisha mchakato wa Maafisa Biashara wanapata mafunzo ya kuwajengea uwezo (capacity building) ambayo itakuwa ni pamoja na kupata mafunzo nje ya nchi na semina mbalimbali ili kusaidia uchumi wa taifa kukua.

Aidha Dkt.Jafo ameziagiza Taasisi zote zinazotoa mada kuwapa maarifa maafisa hao ili kuwajengea uwezo zaidi ili kufanya vizuri katika nafasi na mamlaka walizokuwa nazo.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe.Balozi Dkt.Batilda Buriani amesema kama Mkoa wameendelea na mipango mbalimbali ya kuwasaidia wafanyabiashara kwa kufanya kliniki za biashara na kuchukua changamoto zao na pia amesema kama Mkoa wataendelea kutatua changamoto za wafanyabiashara.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Biashara Wanawake Tanzania (TAWTO) Bi.Elizabeth Swagi amesema miongoni mwa malengo ya kuanzishwa kwa chama hicho ni pamoja na kushauri na kuisadia Serikali kuboresha sheria zinazosimamia biashara na ujasiriamali na kushirikiana na Serikali na Mashirika mbalimbali yanayoshughulikia maendeleo ya wanawake wajasiriamali.