Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

KONGANI YA VIWANDA KUJENGWA ENEO LA NDC MACHAME


Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara imetangaza kuwa eneo la NDC lililopo njia panda ya Machame wilayani Hai litajengwa Kongani ya Viwanda (Industrial Park), baada ya kumpata mshauri mwelekezi kwa ajili ya upangaji wa eneo hilo.

Hatua hiyo imebainishwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), Juni 10, 2026 Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu Swali Namba 559 la Mbunge wa Hai, Mhe. Saashisha Mafuwe aliyetaka kufahamu ni lini eneo hilo la NDC litaachiwa wafanyabiashara ili waanze kulitumia na kuanzisha mji mdogo wa kibiashara mkoani Kilimanjaro.

Akijibu Swali hilo, Waziri Kapinga amefafanua kuwa eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 229.13 chini ya umiliki wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), kwa sasa Serikali imewakodishia wananchi kwa ajili ya shughuli za kilimo wakati taratibu za ujenzi zikiendelea.

Katika Swali la nyongeza, Mhe. Mafuwe amehoji utayari wa Serikali kupokea majina ya wafanyabiashara wa Hai wanaotaka kuendeleza eneo hilo, pamoja na kushirikiana na Halmashauri ili kuoanisha mradi huo na matakwa ya mpango kazi wa wilaya ya Hai.

Waziri Kapinga amejibu kuwa mshauri mwelekezi ana kazi tatu za msingi ambazo ni kuandaa Mpango Kabambe (Master Plan), usanifu wa miundombinu na tathmini ya mazingira, ambapo baada ya hapo watakaa na Halmashauri na kuwapa kipaumbele wawekezaji wa ndani.

Naye Mbunge wa Moshi Mjini Mhe. Ibrahim Shayo, katika Swali dogo la nyongeza amehoji kuhusu mkakati wa Serikali wa kufufua viwanda vilivyokufa katika jimbo lake ambavyo vimesababisha ukosefu mkubwa wa ajira kwa wananchi.

Akijibu Swali hilo, Waziri Kapinga ameeleza kuwa kufuatia maelekezo ya Rais Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kufanya tathmini ya Viwanda vilivyokufa na kuja na mkakati wa kuvifufua, Wizara imeanza kufanya tathmini na tayari baadhi ya Viwanda vikiwemo viwanda vya mbao na kahawa vimeanza kuwekewa mkakati wa kuvifufua kupitia mpango wa miaka sita wa kuhamisha na kufufua Viwanda.