Habari
Kamati ya Waziri Mkuu yaanza kukusanya maoni ya wafanyabiashara Dar es Salaam

Kamati ya Waziri Mkuu yaanza kukusanya maoni ya wafanyabiashara Dar es Salaam
Kamati maalum ya kutatua changamoto za kibiashara nchini iliyoundwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa imeanza kukusanya maoni ya wafanyabiashara kutoka sekta mbali mbali jijini Dar Es Salaam.
Kamati hiyo inaundwa na wajumbe 14 miongoni mwao wakiwemo wajumbe 7 kutoka jumuia ya wafanyabiashara wanaowawakilisha wenzao na wajumbe kutoka Wizara zinazohusika na sekta ya Biashara nchini.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt.John Jingu amesema kuwa kamati hiyo imepewa siku 14 kukamilisha kazi ya kukusanya maoni ya wafanyabishara kote nchini kisha kuwasilisha ripoti hiyo Serikalini kwa ajili ya kutafutiwa ufumbuzi.
Bw. Jingu amepongeza mahudhurio ya wafanyabiashara hao kwa jinsi wanavyotoa maoni yao kwa uwazi na uhuru ili kuwezesha pande zote mbili kufikia muafaka wa kutatua changamoto zilizojitokeza hapo awali na kupelekea wafanyabiashara kufunga maduka yao.
‘’Natoa shukrani zangu za dhati kwa Wafanyabiashara wa Dar es salaam kwa kutuunga mkono na kutupa ushiriakiano wa hali ya juu, hivyo naomba kutoa wito kwa Wafanyabiashara watakaopitiwa na kamati hiyo kote nchini kutoa ushirikiana kwa kamati ili kuwezesha kupata majawabu sahihi na kuleta mapendekezo yanayotakiwa’’
aliongeza Bw.Jingu.
Kwa upande wake katibu wa kamati hiyo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara Dr. Hashil Abdalah amesema kuwa Serikali ya Dkt. Samiah Suluhu Hassan ni serikali sikivu hivyo ipo tayari kuwapatia Wafanyabiashara hao nafasi ya kujadili kwa pamoja kero zao ili tuone nini kifanyike na kupata ufumbuzi yakinifu.
‘’Niwahaidi Watanzania, Mhe. Rais yupo tayari kuwasaidia Wafanyabiashara wote kwani ameonesha nia kubwa na kuguswa zaidi na matatizo yaliyojitokeza na kusababisha mgomo na ndio maana ameituma kamati hii ili kusikiliza kero na kisha kuziwasilisha serikalini kwa maslahi mapana ya nchi na kudumisha uhusiano uliopo baina ya Serikali na Wafanyabiashara nchini.’’
alisisitiza Dkt.Hashil.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Bw. Hamis Livembe alisema kuwa Kikao hicho ni kwa ajili ya kupata Mapendekezo ya nini kifanyike ivyo amewashauri Wafanyabiashara kutoa maoni na kero zao zote zinazowakabili ili Serikali iangalie namna bora ya kuweza kuzifanyia kazi.
Kamati hiyo imepanga kufanya mikutano kwa siku mbili kuanzia tarehe 22 na 23 Mei, 2023 Jijini Dar Es Salaam na kisha itahamia katika kanda mbali mbali za Tanzania Bara na Zanzibar na kuhitimisha kwa kufanya majumuhisho kabla ya kuwasilisha ripoti hiyo kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa