Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

KAPINGA: FCC SIMAMIENI MIKATABA YA WALAJI ILI KUONDOA MASHARTI KANDAMIZI


Tume ya Ushindani (FCC) inahimizwa kusajili na kusimamia mikataba ya walaji ili kubaini na kuondoa masharti kandamizi yanayowekwa na upande mmoja. Hatua hiyo inalenga kulinda haki za walaji katika mikataba ya ununuzi wa bidhaa na huduma mbalimbali.

Vilevile, FCC imeelekezwa kukamilisha utafiti wa soko la biashara mtandao nchini na kuwasilisha mapendekezo yatakayosaidia katika uundaji wa Mkakati wa Biashara Mtandao. Mkakati huo unalenga kuongeza uwazi, kurahisisha uwekezaji, na kuimarisha usalama wa walaji kidijitali.

Maagizo hayo yametolewa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb.), Aprili 2, 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Haki za Mlaji Duniani.

Aidha, Waziri Kapinga ameiagiza FCC kushirikiana na taasisi nyingine za udhibiti, zikiwemo Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Wakala wa Vipimo (WMA), katika kudhibiti ukiukaji wa haki za mlaji na utoaji wa elimu kwa umma.

Pia, amepongeza uanzishaji wa jukwaa la kidijitali la ‘FCC Kiganjani’ kupitia WhatsApp, na kuitaka tume hiyo kuendelea kutoa elimu kupitia mitandao ya kijamii pamoja na kuanzisha klabu mashuleni. Hatua hizi zinalenga kuleta uwazi, kurahisisha uwasilishaji wa malalamiko, kutoa mrejesho wa haraka, na kuongeza uwajibikaji katika masuala ya ushindani na ulinzi wa walaji.

Naye Mwenyekiti wa FCC, Dkt. Aggrey Mlimuka, amesema tume imejipanga kikamilifu kumhudumia mlaji. Alisisitiza kuwa ili kufikia azma hiyo, ushirikiano wa karibu kati ya FCC, Wizara, na mamlaka nyingine za udhibiti ni muhimu katika kudhibiti bidhaa bandia.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa, ameeleza kuwa tume imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu haki na wajibu wa mlaji ili kuwawezesha wananchi kufanya maamuzi sahihi wanaponunua bidhaa na huduma.