Habari
KAPINGA: ITHIBATI YA TBS NI SILAHA YA TANZANIA KUSHINDA SOKO LA SADC NA KIMATAIFA
Kupatikana kwa ithibati ya umahiri wa kimataifa katika mfumo wa ukaguzi wa ISO/IEC 17020 ni hatua kubwa itakayoiondolea Tanzania vikwazo vya kiufundi katika biashara na ni uthibitisho wa weledi na uadilifu wa Serikali katika kudhibiti ubora, kuongeza imani ya wadau kwa bidhaa zinazozalishwa nchini kushindana kwenye masoko ya kikanda na kimataifa bila kutiliwa shaka
Hayo yamesemwa Februari 13, 2026, na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Salvio Kapinga (Mb.), katika hafla ya kihistoria ya kukabidhiwa cheti cha ithibati ya umahiri wa mfumo wa ukaguzi kwa kiwango cha kimataifa (ISO/IEC 17020) kilicgotolewa na Taasisi ya SADCAS kwenda kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri Kapinga amesisitiza kuwa umuhimu wa ithibati hiyo unahakikisha kuwa shughuli za ukaguzi zinazofanywa na TBS zinakidhi vigezo vya kimataifa, hivyo kurahisisha upatikanaji wa masoko, kuimarisha usalama wa bidhaa kwa ajili ya kulinda afya za walaji, na kukuza uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Aidha, Waziri Kapinga amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake thabiti uliowezesha kuwepo kwa mazingira bora ya biashara na uwekezaji ambayo yameimarisha miundombinu ya TBS na mifumo ya udhibiti ili kuhakikisha bidhaa za Kitanzania zinapata thamani stahiki na uwezo wa kushindana kibiashara.
Vilevile, Waziri ameushukuru Umoja wa Ulaya (EU) na Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa (UNIDO) kwa ushirikiano wao wa kimkakati huku akiipongeza na kutoa wito kwa TBS na wadau wa sekta binafsi kuilinda ithibati hiyo kwa "wivu mkubwa", uadilifu wa hali ya juu, na uendelevu wa mifumo ya kiutendaji ili kuvutia uwekezaji na kuhakikisha kuwa Tanzania inabaki kuwa kitovu cha bidhaa bora SADC na duniani kote.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi amebainisha kuwa TBS imekuwa taasisi ya kwanza nchini na ya pili katika ukanda wa Afrika Mashariki kupata ithibati hiyo kutoka SADCAS, ikithibitisha kuwa mifumo ya ukaguzi ya shirika hilo inakidhi vigezo vya kimataifa katika maeneo ya uzalishaji, bandarini na mipakani.
