Habari
Kitengo cha Kuratibu Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Chaanzishwa

Serikali imeanzisha kitengo maalumu kinachoitwa Business Inviroment Unit (BIU) ambacho kitasimamia sekta zote za kibiashara katika utekelezaji wa Mpango wa Kiboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI) ili kubainisha Changamoto na kero zilizopo katika Biashara na kuzitatua kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali zikiwemo za kisera na mamlaka za kodi.
Akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya semina na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Bungeni Dodoma, Naibu waziri Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mh. Exaud Kigahe amesema kuwa MKUMBI unaojulikana kama Blueprint utajikita kusimamia changamoto zote katika sekta mbalimbali zinazolalamikiwa na Wafanyabiashara kuwa na mazingira magumu katika uwekezaji na ulipaji kodi na tozo mbalimbali.
Kigahe amesema kuwa mpango huo ulianza mwaka 2019 baada ya kubaini wafanyabiashara wengi kutoka sekta mbalimbali kukumbana na changamoto nyingi ambazo zinakwamisha kazi zao licha ya kwamba utekelezaji wake ulikuwa haujaanza. "Kama mnavyojua kwa tafiti za mwaka 2020 katika mataifa tuko namba 141 ambayo sio nzuri hivyo tukaona kupitia MKUMBI kuona namna ya kuondoa vikwazo kwenye sekta zote hasa wingi wa tozo ambazo sio za lazima hususani kwenye usafirishaji, kilimo, nishati,maji, na mafuta kitengo hiki kitaratibu na kutatua changamoto hizo" Amesema Kigahe.
Amesema vikwazo vingine kulikuwa na utitiri wa taasisi za udhibiti na muingiliano wa majukumu yao hasa TBS na TFDA hivyo kupitia MKUMBI imepewa jukumu la kubaini changamoto zote kutoka kwa wadau na kuzifanyia kazi
"Leo wabunge wamepata nafasi ya kusikiliza taarifa ya mwanzo ya mwaka wa kwanza ya kutekeleza kutatua changamoto nyingi na tayari kitengo kimeishakuwa na bajeti yao katika utendaji kazi zao na wabunge wetu wametoa maoni yao ya namna ya kuboresha. "Amesema Kigahe.
Akizungumzia manufaa yatakayopatikana kupitia MKUMBI amesema ni pamoja na kusaidia usajili wa kuanzisha biashara ndani ya siku saba kwa mfanyabiashara, kusaidia kuondoa utitiri wa kodi kutoka kwenye taasisi mbalimbali ambazo hazina tija ambazo zimepelekea wengi kufunga biashara bila faida.
Naye Mbunge wa jimbo la Ndanda Cecil David Mwambe ambaye ni miongoni mwa wabunge waliopata semina hiyo amesema kuwa MKUMBI utakuwa na tija kwa Taifa hasa kuwasaidia wafanyabiashara kuondoa vikwazo,mesema licha ta jitihada zilizofanya kuna haja ya kukaa na wawekezaji wa viwanda kuongea nao namna ya kupunguza gharama za uzalishaji ambazo urudishwa kwa wananchi.