Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

TATHIMINI YA MAHITAJI YA SHERIA YA KUSIMAMIA BIASHARA YATAKIWA KUFANYIKA HARAKA


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kufanya tathimini ya mahitaji ya Sheria ya kusimamia Biashara kwa haraka ili kuimarisha usimamizi wa sekta hiyo nchini kwa lengo la kukuza biashara, kuongeza ajira, Pato la Taifa, kukuza uchumi shindani wa viwanda na kutimiza Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Hayo yameagizwa Februari 11, 2026 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe.Deodatus Mwanyika wakati wa Mafunzo kwa Wajumbe wa Kamati hiyo kuhusu Sera ya Taifa ya Biashara ya mwaka 2003 Toleo la 2023.

Mwanyika amesema ni muhimu tathmini ya kuandaa sheria ya biashara ikamilishwe kwa wakati ili kubaini kama mapendekezo yaliyotolewa yataisaidia kufikia malengo ya utekelezaji wa Sera hiyo

Aidha, Wajumbe wa Kamati hiyo walipata fursa ya kutoa maoni na mapendekezo mbalimbali yaliyolenga kuboresha utekelezaji wa Sera hiyo kwa ufanisi na kuendelea kushughulikia changamoto zinazoibuka katika utekelezaji huo.

Naye, Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga akiwa ameambatana na Katibu Mkuu Mhe. Balozi Waziri Rajabu Salum, Naibu Katibu Mkuu Bw. Aristide Mbwasi, Menejimenti ya Wizara na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara yake, ameihakikishia Kamati hiyo kuwa Wizara yake itayafanyia kazi maoni na mapendekezo yote yaliyotolewa na Kuwa Mikakati iliyowekwa kwa ajili ya kutekeleza Sera hiyo kwa kasi na kwa ufanisi ili kupata Matokeo chanya yanayotarajiwa katika kuendeleza Sekta ya Viwanda na Biashara na kukuza uchumi kwa ujumla.

Akiwasilisha taarifa hiyo, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga (Mb), Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara, Bw.Needpeace Wambuya, amesema Wizara imependekeza kutungwa kwa sheria mpya ya biashara au kufanyiwa maboresho kwa sheria zilizopo, ambapo uchambuzi wa awali tayari umefanyika na mchakato wa kupanua mawanda unaendelea.