Lindi Kufufua na Kuanzisha Viwanda vipya.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Mb) amesema Wizara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina pamoja na Mkoa wa Lindi itaendelea kutafuta Wawekezaji Sahihi wenye nia ya kufufua viwanda vilivyosimama au kuanzisha viwanda vipya katika Mkoa wa Lindi ili kuongeza ajira, Pato la Taifa na kukuza uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Waziri Jafo ameyasema hayo Septemba 21, 2024 alipokuwa, akihitimisha Ziara Maalum katika Mkoa wa Lindi iliyolenga kukagua utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo katika Awamu ya Sita chini ya kauli mbiu isemayo "Rais Samia na Maendeleo Wasikie na Waone" iliyoanza tarehe 17 - 21/09/2024 Mkoani humo.
Akiweka Jiwe la Msingi katika Miradi mbalimbali ya Maendeleo katika sekta ya afya, elimu, maji, ujenzi, uzalishaji pamoja na kuongea na Wananchi wakati wa ziara hiyo, Waziri Jafo amesema Mkoa wa Lindi umetekeleza miradi hiyo kwa ufanisi na kuutaka kuendelea kusimamia miradi hiyo ikamilike kwa wakati na ianze kutoa huduma kwa umma.
Aidha, Waziri Jafo, amewasisitiza Wananchi wa Mkoa huo kuhakikisha wanawapeleka watoto wote wenye mahitaji maalum katika shule zilizojengwa kwa ajili yao ili wapate elimu kama haki yao ya msingi ya kijamii.
Vilevile Waziri Jafo ameendelea kuwasisitiza Wananchi wa Mkoa wa Lindi kujiunga na kutumia vyama vya ushirika, kuhifadhi mazao yenye ubora kwenya Ghala zinazotumia Mfumo wa Stakabadhi Za Ghala ili kuongeza thamani ya mazao na kupata faida.