Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Mafunzo Haya ni Kwa Manufaa ya Jamii


Mafunzo Haya ni Kwa Manufaa ya Jamii

Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah amewataka Maafisa kutoka Wizara hiyo kutumia vizuri ujuzi watakaoupata katika Mafunzo ya Uandaaji wa Maandiko ya Miradi kwa manufaa ya Jamii.

Dkt. Abdallah amesema hayo leo Septemba 23, 2024 wakati akifungua Mafunzo ya siku tano ya Uandaaji wa Maandiko ya Miradi kwa Maafisa wa Taasisi 13 zilizopo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ambapo alisema lengo la mafunzo hayo ni kupata ujuzi endelevu kwa ajilii ya kuboresha maandiko ndani ya Wizara.

“Mafunzo haya mnayapata kwa niaba ya Taasisi zenu lakini mwisho wa siku mfanye kazi kwa pamoja, hii ni dhamana kubwa kwenu, utekelezaji wa shughuli mbalimbali kwenye Wizara unategemea uwezo wa watu na rasilimali fedha, hivyo tunategemea maandiko yaliyoandikwa kitaalam ili yaweze kupata ufadhili kwa manufaa ya jamii yote ya Tanzania,” alisema Dkt. Abdallah.

Alisema, kufanyika kwa mafunzo hayo ni matokeo ya juhudi iliyoratibiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uandaaji Miradi, ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Prof., Edda Tandi Lwoga pamoja na timu yake baada ya kuona ombwe na kuchukua hatua ya kulifanyia kazi akishirikiana na Idara ya Fedha na Mipango ya Wizara hiyo.

Kwa upande wake Prof., Lwoga, alisema aliona haja ya watumishi kujengewa uwezo na kwamba jukumu hilo lilianza rasmi mwezi Machi, 2024 na mpaka sasa wameshaandika maandiko 13 wakilenga zaidi kwenye viwanda vidogo vidogo, biashara za wamachinga na kuboresha miundombinu katika miradi ya uwekezaji na maeneo ya teknolojia za ubunifu.