Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Makamu wa Rais awakaribisha wawekezajina wafanyabiashara kutoka Umoja wa Ulaya


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amewakaribisha wawekezaji kutoka Umoja wa Ulaya kuwekeza nchini katika sekta za Kilimo, Usafirishaji, Nishati, Tehama, Utalii na katika Viwanda vya kuongeza thamani kwa kuwa Serikali inahitaji kufungua zaidi sekta hizo ili kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 23 Februari 2023 wakati akifungua Kongamano la Kwanza la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam.

Ameongeza kuwa Tanzania ipo katika maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa kwa miaka mingine 25 ambayo inalenga kubadilisha uchumi wa Taifa kutoka katika hali ya uchumi wa kati wa chini hadi kufikia uchumi wa kati wa juu ambapo kwa kiasi kikubwa unahitaji biashara na uwekezaji.

Pia Makamu wa Rais amewahakikishia wawekezaji hao mazingira mazuri na salama ya uwekezaji na biashara hapa nchini kwa kuzingatia juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini ikiwemo kuweka sera imara na zinazotabirika, sheria na taratibu rafiki, kuboresha huduma za kijamii, kuimarisha demokrasia, usawa wa kijinsia na utawala wa sheria, kuendeleza miradi mikubwa ikiwemo ya nishati na miundombinu, uchukuzi na usafirishaji.

Amesema ushirikiano huo unaambatana na matarajio ya Tanzania ya kuwa sio tu kitovu cha biashara cha kikanda bali pia ghala la chakula ulimwenguni.

Ameongeza kwamba uwekezaji utanufaika na soko kubwa la ndani la watu milioni 61.7, soko la kikanda la Jumuiya ya Afrika Mashariki la watu zaidi ya milioni 177, Soko la Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) la zaidi ya watu milioni 300 pamoja na Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika (AfCFTA) linalojumuisha nchi 55 za Afrika zenye soko lisilopungua watu bilioni 1.4.

Makamu wa Rais ametoa wito kwa Kongamano hilo kuwa mwanzo wa makongamano mengine yajayo na kuwa na mijadala ya wazi juu ya fursa, hofu na vikwazo vinavyozuia maendeleo ya haraka katika kuchochea uwekezaji na biashara baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya.

Pia amewahimiza wafanyabiashara nchini Tanzania kutumia fursa ya kongamano hilo kujifunza, kubadilishana uzoefu, kufahamiana na wawekezaji mbalimbali na kutafuta fursa za kushirikiana na kuingia makubaliano ya kibiashara.