Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA, GAIN NA GALAXY WAZINDUA MRADI KUU WA MAZIWA SHULENI NA SOKO


Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Shirika la Global Alliance for Improved Nutrition (GAIN) na Galaxy Food and Beverage Ltd, imetambulisha mradi wa kuimarisha soko la maziwa nchini, mradi utakaowanufaisha zaidi ya wanafunzi 120,000 kwa kupeleka huduma ya maziwa shuleni na wafugaji 7,000 kwa miaka miwili katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam na Kilimanjaro.

Mradi huo unafadhiliwa kwa na Shirika la Global Alliance for Improved Nutrition (GAIN) kwa asilimia 50 na Galaxy Food and Beverage Ltd asilimia 50, umezinduliwa Oktoba 8, 2025 katika Ukumbi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), jijini Dodoma, ukihudhuriwa na Wizara ya Viwanda na Biashara, wadau wa lishe, mashirika ya maendeleo pamoja na taasisi mbalimbali za serikali.

Akizungumza wakati wa ufunguzi, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Nyango E. Mbogora, amesema mradi huo unalenga kuongeza upatikanaji wa lishe bora kwa wanafunzi wa shule za msingi kupitia maziwa yenye virutubisho na salama kwa afya.

Kwa mujibu wa maazimio ya kikao hicho, vigezo vya kuchagua shule zitakazonufaika na mradi huo vitahusisha shule zisizo na mpango wa maziwa, shule zenye changamoto za ufaulu na utoro, pamoja na maeneo yenye upatikanaji rahisi wa huduma za umeme kwa ajili ya uhifadhi wa bidhaa.

Dkt. Winfrida Mayilla, Mkuu wa Programu wa GAIN, amesema matarajio ya mradi huo ni kuhakikisha wanafunzi wapatao 128,553 wanakunywa maziwa ya yogurt shuleni, kuchakata lita 29,000 za maziwa kwa siku na kuongeza kipato cha Watanzania kupitia thamani ya bidhaa za maziwa.

Kwa upande wake, Meneja wa Viwanda wa Galaxy Food and Beverages Ltd, Bw. Fidelis Madzorera, ameeleza kuwa mradi huo utazingatia usalama wa mazingira kwa kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa kupitia matumizi ya nishati ya jua katika vituo 22 vya ubaridi vitakavyoanzishwa.

Aidha, Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Bw. Joseph Semu, alisema Tanzania huzalisha lita bilioni 4.01 za maziwa kwa mwaka, huku lita bilioni 1 pekee zikichakatwa, hivyo mradi huo unatarajiwa kuongeza mnyororo wa thamani wa maziwa nchini na kuongeza kipato kwa wafugaji.