Habari
MWELEKEO SAHIHI NA WENYE TIJA KWA WAKULIMA NI KUPITIA MFUMO WA STAKABADHI GHALANI – NAIBU WAZIRI KIGAHE.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe ameeleza kuwa Mwelekeo sahihi na wenye manufaa na tija kwa wakulima ni kupitia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani na ndipo kuna uhakika wa wakulima kufaidika na kilimo na uhakika wa soko la mazao yao.
Mhe. Kigahe ameyasema hayo katika mkutano uliowakutanisha wakulima wa mazao yanayotumia Mfumo huo wa Mkoa wa Mtwara na Kamati Maalum ya Bunge inayofuatilia na kujengewa uelewa juu ya Mfumo wa Stakabadhi Ghalani ili kujua mwenendo wa mfumo huo kwa mazao ya Korosho, Ufuta, Soya, Mbaazi, kahawa na mazao mengine.
“Mwelekeo sahihi na wenye manufaa na tija kwa wakulima ambao ni Zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania ni kupitia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani, huko ndipo tuna uhakika wa wakulima watafaidika pia uhakika wa soko la mazao yao” amaeeleza Mhe. Exaud Kigahe, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara
Amesema kuwa amefarijika sana na wana Mtwara kwa kazi kubwa inayofanyika kupitia vyama vya ushirika ambavyo vimeimarishwa na ameona baadhi ya vyama vinarejesha sehemu ya faida inayotokana na mfumo huo kufanya shughuli za kijamii mfano kujenga barabara, vyumba vya madarasa na vituo vya afya.
Aidha, Mhe. Kigahe ametoa wito kwa Vyama vya Msingi kuona namna ya kuanza kujiteagemea kwa kutatua changamoto ndogo ndogo za wakulima mfano mkulima anapopeleka mazao yake ghalani wakati anasubiria malipo wanaweza kufanya utataratibu wa kumkopesha ili atatue matatizo yake na pale fedha zinapokuja ndipo anakatwa na nyingine iliyobaki anawekewa kwenye akaunti yake ya benki.
Kwa upande wake, Mhe. Rashid Abdallah Shangazi (Mb) Mbunge wa Jimbo la Mlalo na Mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya Bunge ametoa wito kwa vyama vya msingi vya mkoa wa Mtwara kujifunza kwa vyama vingine vya msingi kama Mbinga ambao wamefanya uwekezaji wa kiwanda cha kubangua kahawa, pia vyama vingine vya ushirika na AMCOS ambao wametoa sehemu ya asilimia ya faida kwenye jamii kwa ajili ya kujenga miundombinu na kuchangia kwenye shughuli za Maendeleo.