Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

MAANDALIZI YA MKUTANO KATI YA TANZANIA NA ZAMBIA


Maandalizi ya Mkutano wa Kamati ya Pamoja ya Biashara (Joint Trade Committee – JTC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Zambia yameanza ngazi ya watalaam Mei 04, 2026 mjini Tunduma mkoani Songwe kwa lengo la kujadili masuala ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili ikiwemo uondoshwaji wa vikwazo vya ushuru na visivyo vya ushuru vinavyowakabili wafanyabiashara wa nchi hizo mbili.

Mkutano huo wa siku nne kuanzia Mei 4 hadi Mei 7, 2026 umeanza katika ngazi ya Wataalamu ambapo wanajadili na kuandaa ajenda zitakazowasilishwa kwa Makatibu Wakuu watakaokutana Mei 6, 2026 kabla ya kuhitimishwa kwa Mkutano wa Mawaziri utakaofanyika Mei 7, 2026.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, katika ngazi ya Wataalamu Mkurugenzi wa Mtangamo wa Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Bishara - Tanzania Bw. Ombeni Mwasha (Mwenyekiti wa kikao) amesisitiza kuhusu umuhimu wa majadiliano ya uwazi na kina ili kupata suluhisho la kudumu dhidi ya changamoto zinazoathiri ustawi wa sekta ya biashara kati ya pande hizo mbili.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa katika Wizara ya Biashara na Viwanda - Zambia na mwenyekiti mwenza wa mkutano huo Dkt. Simon Ng’ona ameeleza kuhusu utayari wa Nchi hiyo wa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kutatua changamoto zilizopo, akibainisha kuwa hatua hiyo itarahisisha na kuongeza mwingiliano wa bidhaa, huduma na watu, pamoja na kuchangia ukuaji wa maendeleo ya uchumi wa kanda.

Mkutano wa JTC pamoja na muasula mengine unalenga kuunganisha juhudi za pamoja katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Zambia, kwa kujadili na katatua changamoto mbalimbali ikiwemo maboresho ya sera, kurahisisha taratibu za forodha, na kuendeleza miundombinu ya kimkakati ili kuongeza kiwango cha biashara, kuvutia uwekezaji na kuchochea maendeleo ya mataifa hayo mawili na ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).