Habari
PROF. MKUMBO AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA UONGOZI WA BENKI YA NMB
Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo amezitaka taasisi za benki nchini kuongeza huduma ya utoaji wa mikopo kwa wajasiriamali nchini ili kuwasaidia kukua na kukuza mitaji yao, hayo ameyasema leo tarehe 8 Novemba, 2021 alipokutana na uongozi wa benki ya NMB na kujadiliana changamoto mbalimbali zinazohusu wafanyabiashara nchini.
Mhe. Mkumbo ameishukuru benki ya NMB kwa mabadiliko makubwa yaliyofanyika ya kiutendaji ambayo yamepelekea benki kuwa na huduma nzuri na bora kwa watanzania.
Mhe. Mkumbo amesema kuwa kazi kubwa ya wizara ya Viwanda na Biashara ni kuratibu na kusimamia uendelezwaji wa Viwanda nchini kwa kushirikiana na sekta binafsi ambapo idadi ya Viwanda nchini imeongezeka na kufikia 80,969 ambapo amebainisha kuwa Viwanda hivi nchini vinakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya uendelezwaji wa biashara zao hasa kwa Wajasiriamali wadogo ambao serikali imedhamiria kuhakikisha wanasaidiwa kwa karibu.
Mhe. Mkumbo ameeleza kuwa wizara imejipanga katika uendelezwaji wa miradi mikubwa ya Liganga na Mchuchuma, Ujenzi wa Mitaa ya Viwanda, mradi wa Kurasini, mradi wa magadi soda wa Engaruka na miradi mingine ya kimkakati ambapo kupitia mabenki yetu nchini yatawawezesha wawekezaji wengi zaidi kutoka nje na ndani ya nchi watakaowekeza katika miradi mbalimbali.
“Wajasiriamali nchini ni lazima watambulike ili iwe rahisi kuwasaidia huduma mbalimbali hasa za upatikanaji wa fedha, bajeti ya serikali ambayo ni zaidi ya trilioni 31, asilimia 40 ya bajeti hiyo ni fedha za maendeleo hivyo mabenki yetu yanatakiwa kuhakikisha fedha hizi zinafika kwa wafanyabiashara wetu kupitia miradi mbalimbali ziingie katika mzunguko kukuza uchumi wa nchi yetu na kusaidia kuongeza mabilionea wa kitanzania wengi zaidi” Amesema Prof. Mkumbo.
Mhe. Mkumbo amesema kuwa Wizara kupitia SIDO ilianzisha mfuko wa NEDF mahsusi kwa ajili ya kusaidia wajasirimali wadogo hivyo ametoa wito kwa taasisi za kibenki nchini kujitanua zaidi katika upande wa kuwasaidia wajasiriamali na kutanua mtandao wa huduma ndani na nje ya nchi mfanyabiashara aweze kufanya miamala kwa urahisi na kwa haraka.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa benki ya NMB nchini Bi. Ruth Zaipuna amesema kuwa benki ya NMB ni mhimili muhimu sana katika uendelezwaji wa Viwanda na Biashara nchini hasa katika kuhakikisha wanaendelea kutoa huduma bora kwa wafanyabiashara nchini.
Bi. Ruth amesema kuwa Benki ya NMB ina uwezo mkubwa sana wa kuwahudumia watanzania wafanyabiashara wakubwa na wadogo kuhakikisha wanapata mikopo, Ameongeza kwa kusema kuwa benki hiyo ina matawi zaidi 226, wakala wa NMB, ATM na huduma za kibenki kupitia mtandao.
Bi. Ruth ameongeza kuwa benki ya NMB imejikita zaidi katika kutoa ujuzi na kuwajengea uwezo wawekezaji na wafanyabiashara nchini na kuwaingiza katika mfumo rasmi wa kibenki kwa ajili ya kupata mikopo, usalama wa fedha zao.
Aidha amesema kuwa benki ya NMB pia imekuwa ikitoa elimu kwa wafanyabiashara kuweka taarifa za biashara na hesabu zao vizuri ili kusaidia muendelezo wa biashara husika hata pale ambapo mwanzilishi wa biashara hiyo anapokuwa hayupo.
Bi. Ruth amemaliza kwa kusema kuwa benki ya NMB inasapoti mfumo wa “Warehouse Receipt System” unaosimamiwa na Bodi ya Maghala nchini ambapo benki inasaidia ujenzi wa maghala ambayo ni ya kisasa yanayokubalika kimataifa katika uhifadhi wa bidhaa hasa za kilimo.