Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

RAIS DK.MWINYI AZITAKA TAASISI ZA SERIKALI KUONDOA URASIMU KATIKA BIASHARA NCHINI


RAIS DK.MWINYI AZITAKA TAASISI ZA SERIKALI KUONDOA URASIMU KATIKA BIASHARA NCHINI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi amezitaka taasisi zinazosimamia biashara kuhakikisha zinaondoa urasimu na zinaweka mazingira bora ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini

Ameyasema hayo Julai 13, 2023 wakati akifunga Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yaliyofanyika uwanja wa Maonesho wa Mwalimu Julius Nyerere  Jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 28, hadi 13,Julai 2023.

Aidha, Rais Dkt. Hussein Mwinyi ametoa wito kwa Watanzania kuwa tayari kujifunza teknolojia mpya watakazozitumia kukuza biashara zao kutokana na Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.

Aidha, Rais Dk.Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zitaendelea kushirikiana katika kuhamasisha ukuaji wa biashara na uwekezaji kwa kufanyia kazi maoni ya wafanyabiashara nchini na kuwezesha taasisi  za Serikali kuwa na mifumo inayosomana ili  kupunguza gharama zisizo za lazima na kuondoa utitiri wa tozo katika biashara nchini.

Naye, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda wa Zanzibar Mhe Omar Said Shaaban amesema, Zanzibar inaendelea na mipango yake ya kuandaa maonesho ya kudumu ya biashara ambayo yatakuwa yakifanana na maonesho ya Sabasaba

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) Bi Latifa Khamis amesema Maonesho hayo yaliyoshirikisha kampuni 3500 ikiwemo kampuni  267 kutoka Nchi 17 na kutembelewa na wananchi takribani Milioni 3 na yalitoa ajira za muda takriban 11,687.

Aidha, amesema mauzo ya bidhaa zenye thamani ya bilioni 3.8. yamefanyika wakati wa maonesho hayo na bidhaa za thamani ya bilioni 16.98 zimeuzwa nje ya nchi na hati za makubaliano tisa(9) katika maeneo mbalimbali ikowemo kilimo na elimu zimetiwa saini kupitia Mkutano wa wafanyabiashara kwa wafanyabiashara.