Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SERIKALI HAITAVUMILIA WAFANYABIASHARA WANOPANDISHA BEI ZA BIDHAA KIHOLELA


Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dk, Ashatu Kijaji  amesema Serikali haitavumilia tabia ya wafanyabiashara wachache wenye dhamira ovu ya kuwaumiza wananchi kwa kujiamulia kupandisha bei za bidhaa bila kufuata utaratibu kwa manufaa yao binafsi kwa kuwa Serikali inajukumu la msingi la kusimamia ushindani wa haki kwenye soko kwa kudhibiti mienendo hadaifu au kandamizi ya wazalishaji wa bidhaa na wafanyabiashara wanaopandisha holela wa bei za bidhaa nchini.

Waziri Kijaji ameyasema hayo alipokuwa akitoa taarifa ya uchunguzi uliofanywa na FCC, kuhusu uhaba na kupanda kwa bei za vinywaji baridi uliotokea Oktoba hadi Januari 2022 ulitokana na kutopatikana kwa sukari ya viwandani sababu ya ukosefu wa Makasha ya kusafirishia shehena ya s ukari hiyo kuja hapa nchini uliojitokeza duniani kote kutokana na athari za UVICO-19, kwa Waandishi wa Habari mara baada ya kutembelea kiwanda cha Jambo Food Products kilichopo Mkoa wa Shinyanga Januari 23, 2022kuangalia hali ya uzalishaji wa bidhaa za mbalimbali hususani vinywaji baridi.

Aidha Waziri kijaji aliwahakikishia watanzania kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa Sukari hiyo ya viwandani inapatikana kwani hadi sasa tani 25,000 ya sukari ya viwandani imeingia nchini kupitia bandari ya Dar es salaam na inaendelea kupokelewa kwa kuwa Sukari hiyo kwa sasa inasafirishwa kwa njia ya mbadala ya ufungashaji shehena usiotumia makasha (containers), yaani break-bulk.

Akielezea hatua nyingine ambazo Serikali imechukua ili kutatua changamoto hiyo, Waziri Kijaji amezielekeza Mamlaka na Taasisi za Serikali zikiongozwa na Tume ya Ushindahi (FCC) zilizopewa dhamana ya kusimamia mienendo ya masoko ya bidhaa kutekeleza wajibu huo kikamilifu na kwa umakini mkubwa ili kudhibiti mienendo hadaifu au kandamizi ya wazalishaji wa bidhaa na wafanyabiashara kwenye soko ikiwa ni pamoja na upandishaji holela wa bei za bidhaa nchini.

Aidha, Waziri Kijazi amewaelekeza Maafisa Biashara wa Mikoa kote nchini waendelee kufuatilia kwa karibu mwenendo wa bei za bidhaa mbalimbali kwenye maeneo yao na kuwasilisha taarifa hizo mara kwa mara Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, kupitia Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa, ili itakapobidi hatua stahiki zichukuliwe kwa wakati kwa kuwa licha ya kuadimika kwa Sukari ya viwandani, wazalishaji wa vinywaji baridi hawakupandisha bei, isipokuwa mawakala wa usambazaji na wafanyabiashara ndiyo waliopandisha bei, na kuonya tabia hiyo isijirudie tena na watakaobainika watachukuliwa hatua.

Pia Waziri Kijaji amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua za kuongeza ufanisi katika uondoshaji wa shehena bandarini, kuboresha usafirishaji kwenye barabara kuu na kuimarisha upitishaji wa mizigo mipakani  kwa kuwa imeanzisha mfumo wa utoaji wa vibali vya kuagiza sukari ya viwandani kwa njia ya mtandao ili vibali hivyo vipatikane kwa wakati na bila usumbufu wowote na kuhakikisha wazalishaji hawaishiwi malighafi hiyo muhimu ili kuondokana na changamoto ya uingizaji sukari ya viwandani hiyo.  

Dkt Kijaji pia amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara na kuwekeza nchini kwa lengo la kujenga uchumi imara wa viwanda ikiwa ni pamoja na kuhamasisha na kuvutia uwekezaji katika uzalishaji wa sukari ya viwandani hapa nchini ili kuondoa utegemezi wa kuagiza sukari hiyo kutoka nje.

“Natoa wito kwa wawekezaji kuja hapa nchini kuwekeza viwanda vya Sukari ya viwandani, sababu kuna maeneo mengi yametengwa kwa ajili ya uwekezaji, hali ambayo itasaidia kutotokea tena tatizo la kuadimika kwa Sukari hiyo, sababu itakuwa ikizalishwa hapa nchini na siyo kuagiza nje ya nchi” alisema Dkt Kijaji.

Awali kabla ya ziara katika kiwanda hicho akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama Mkoa, Waziri kijaji alitembelea ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga Bi Sophia Mjema na kupata taarifa ya maendeleo ya sekta ya Uwekezaji Viwanda na Biashara pamoja na changamoto mbalimbali ambazo amesema kuwa Serikali itaendelea kuzishughulikia ili kuweka mazingira bora ya uwekezaji na ufanyaji Biashara katika mkoa huo.