Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SERIKALI YA AWAMU YA SITA YAWEKA MKAZO KUJENGA UCHUMI JUMUISHI KWA WANAWAKE NA VIJANA


Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mkazo katika kujenga uchumi jumuishi unao wajumuisha wanawake na vijana kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

Aidha, imechukua hatua mbalimbali za kisera na kiutendaji ili kuimarisha ushiriki wa wanawake katika shughuli za kiuchumi na kutaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa 30% ya zabuni za manunuzi ya umma zinatengwa kwa ajili ya makundi maalum ikiwemo wanawake vijana na watu wenye mahitaji maalum hatua iliyofungua fursa kubwa kwa wanawake kushiriki kikamilifu katika zabuni za Serikali jambo linalosaidia kuongeza kipato pamoja na kukuza biashara zao.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga (Mb), Machi 28, 2026 jijini Dar es Salaam katika Sherehe za miaka 20 ya Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) iliyohusisha ugawaji wa tuzo za Viwanda na Biashara kwa
wanawake Wajasiriamali.

Aidha, amesema kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita TWCC imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kukuza ujasiriamali wa wanawake na kuimarisha ushiriki wao katika maendeleo ya kiuchumi ya nchini.

Ameipongeza TWCC kwa kuwawezesha wanawake na vijana kuwa vinara katika kunufaika na fursa za soko huru la bara la Afrika ambapo wanawake na vijana wamewezeshwa kushiriki kikamilifu katika biashara za kikanda na makundi hayo yamefanikiwa kuuza bidhaa katika soko hilo zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni tisa (9) ikiwa ni miaka minne tangu Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuteuliwa kuwa kinara wa ushirika wa wanawake na vijana katika soko huru la bara la Afrika mwaka 2022.

Kwa upande wake rais wa TWCC CPA Mercy Sila amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha mazingira ya biashara, akibainisha kuwa maboresho ya Serikali katika upatikanaji wa mitaji kupitia madirisha ya wanawake benki na mifuko ya uwezesheji yamepunguza changamoto za masoko na fedha zilizokuwa zikiwakabili.