Habari
WAFANYABIASHARA WADOGO MIPAKA YA TANZANIA NA MALAWI KUNUFAIKA NA MKATABA WA STR
Wafanyabiashara wadogo wanaofanya biashara katika mipaka ya Tanzania na Malawi kunufaika na Mfumo wa kurahisisha na kuimarisha biashara za Wafanyabiasha wadogo wenye mitaji isiozidi dola 2000 zinazofanyika katika mipaka ya
Tanzania na Malawi (Simplified Trade Regime (STR) hususan katika Mpaka mkubwa wa Kasumulo na Songwe.
Makubalino hayo ni moja ya maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye mara zote anapenda masuala ya biashara yawanufainishe Vijana na Wanawake ambao hufanya shughuli za biashara kila siku.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Judith Kapinga wakati wa hafla ya kusaini Mkataba wa makubaliano baina ya nchi ya Tanzania na Malawi Februari 16, 2026, Jijini Lilongwe-Malawi.
Waziri Kapinga amesema Mkataba wa makubaliano hayo ni muhimu kwa wafanyabiashara hususani vijana na wanawake kwani utarahisisha ufanyaji biashara na kupunguza urasimu ambao ulikuwepo awali pamoja na kuwa na utaratibu wa kupata huduma kwa haraka ikiwemo ujazaji fomu ya uasili papo hapo na kuendelea na biashara kwa upande wa pili.
Amesema Mkataba huo unajunuisha Mfumo maalum wa biashara unaolenga kurahisisha taratibu za forodha na kupunguza vikwazo visivyo vya kikodi (NTBs) kwa wafanyabiashara wadogo wanaofanya biashara za kuvuka mipaka ya Tanzania na Malawi (Cross Border Trade).
Aidha, amebainisha kuwa Mkataba huo uliotiwa saini unahusisha Mfumo STR ambao utaruhusu Wafanyabiashara wadogo kusafirisha bidhaa zilizoainishwa kwenye Mkataba huo kwa kutumia nyaraka chache, fomu rahisi za kiforodha na za uasili wa
bidhaa kwa kuzingatia kiwango maalum cha thamani ya bidhaa kilichowekwa katika Mkataba bila kupitia taratibu ndefu za kawaida za forodha
Waziri Kapinga pia amesema kusainiwa kwa Mkataba huo baina ya nchi hizo kutakuza biashara halali mpakani ambapo Wafanyabiashara wadogo watahamasika kufanya biashara kwa kufuata taratibu rasmi badala ya njia zisizo rasmi, Kupunguza gharama za biashara, Kuongeza mapato ya Serikali na Kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Malawi.
