Habari
TANZANIA NA MAREKANI KUIMARISHA USHIRIKIANO WA BIASHARA
Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji ili kuvutia Wawekezaji kutoka Marekani kuja kuwekeza nchini kutumia maeneo maalum ya uwekezaji (SEZ) ambayo yanavivutio vingi vya kikodi na miundombinu rafiki kwa viwanda.
Hayo yamesemwa Februari 12, 2026, na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Aristides Robert Mbwasi, wakati wa hafla ya chakula cha jioni ya kutoa shukrani iliyoandaliwa na Chemba ya Biashara ya Marekani nchini Tanzania (AmCham) katika Hoteli ya Hyatt Regency, Dar es Salaam.
Bw. Mbwasi, ambaye alimwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Salvio Kapinga, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejikita katika kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na kuiwezesha Sekta binafsi kufanya kazi kwa urahisi na ufanisi na Kitaya Tanzania kuwa kitovu cha viwanda na biashara katika ukanda wa Afrika.
Aidha, amewahimiza Wawekezaji kutumia fursa ya Soko la Sheria ya Ukuaji na Fursa kwa Afrika (AGOA) katika sekta za nguo, ngozi, na usindikaji wa mazao ya kilimo lililoongezewa muda wa mwaka mmoja hadi Desemba 2026.
Bw. Mbwasi pia amebainisha kuwa Serikali imepanga kuongeza thamani ya bidhaa zinazouzwa nje ili kuongeza Mauzo ya bidhaa kutoka Tanzania kwenda Marekani kwa kuwa Takwimu zinaonesha kuwa kuanzia mwaka 2016 hadi 2024, urari wa biashara umekuwa ukiinufaisha zaidi Marekani, huku Tanzania ikirekodi nakisi (trade deficit) ya kati ya Dola za Marekani milioni 195 na milioni 354.5.
Vilevile, amebainisha kuwa Tanzania inaendelea kurahisisha taratibu za udhibiti, kuongeza uwazi, na kupunguza gharama za uendeshaji biashara ili kuvutia mitaji katika sekta za nishati safi, madini, na uchumi wa kidijitali.
Vilevile, Bw. Mbwasi amewahakikishia wafanyabiashara wa ndani na nje ushirikiano katika kukuza mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji nchini Tanzania.
