Habari
SEKTA YA HUDUMA NI UTI WA MGONGO WA UCHUMI WA TANZANIA, INACHANGIA ASILIMIA 45 YA PATO LA TAIFA

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara Wizara ya Viwanda na Biashara Bw. Sempeho Manongi, amesema Sekta ya huduma inachangia takribani asilimia 45 ya Pato la Taifa la Tanzania kwa mwaka 2024, ikiongozwa na biashara, uchukuzi, huduma za kifedha, TEHAMA, elimu na utalii.
Amebainisha hayo katika hotuba yake akifungua warsha ya kuwajengea uwezo wadau wa biashara ambayo imeandaliwa na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) Oktoba 09,2025 jijini Dar Es Salaam.
Amesema sekta ya huduma ni uti wa mgongo wa uchumi wa kisasa wa Tanzania na kichocheo kikuu cha ukuaji na ajira.
Amesema sekta ya utalii pekee iliingiza zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 3.3 mwaka 2023, na kuajiri zaidi ya Watanzania milioni 1.5 moja kwa moja na kwa njia zisizo za moja kwa moja.
Ameongeza kuwa sekta ya TEHAMA, inayoendeshwa na ubunifu wa kidijitali na muunganisho wa simu, inachangia karibu asilimia mbili ya Pato la Taifa, huku sekta ya huduma za kifedha ikiendelea kuimarisha ushirikishwaji wa kifedha, na kwa sasa inafikia zaidi ya asilimia 75 ya watu wazima kupitia mifumo ya simu na dijitali.
Manongi amesema mauzo ya huduma za Tanzania nje ya nchi yanakua hasa katika utalii, usafiri, na huduma za kitaaluma sehemu ya mauzo ya huduma katika mauzo ya nje inabaki chini ya asilimia 25, ikilinganishwa na zaidi ya asilimia 40 katika uchumi wa juu.
Bw.Manongi amesema warsha hiyo itatoa moduli za vitendo kuhusu mikakati ya kuingia sokoni, uzingatiaji wa udhibiti, utoaji zabuni, na kuendeleza mipango ya soko la nje, ambayo yote ni muhimu kwa kufungua fursa za usafirishaji wa huduma.
Ameongeza kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki imepata mafanikio makubwa katika kurahisisha biashara ya huduma chini ya Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki, ikijumuisha sekta saba za kipaumbele zikiwemo biashara, mawasiliano, usambazaji, elimu, fedha, utalii na huduma za usafiri.