Habari
TARIME KUNUFAIKA NA KIWANDA KIKUBWA, KUKUZA BIASHARA MIPAKANI
Serikali inaendelea kufanya tathmini ya uwezekano wa kujenga kiwanda cha kimkakati katika Wilaya ya Tarime mkoani Mara ili kukuza uchumi wa eneo hilo na Taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb), bungeni Jijini Dodoma Aprili 01 2026 wakati akijibu swali la Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali kuhusu ujenzi wa kiwanda hicho.
Amesema Wilaya ya Tarime ina nafasi kubwa ya kunufaika na uwekezaji huo kutokana na ukaribu wake na nchi jirani ya Kenya pamoja na uwepo wa shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi na uchimbaji madini.
Amesema baada ya kukamilika kwa tathmini hiyo, Serikali itahamasisha wawekezaji kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kimkakati, hatua itakayosaidia kuongeza ajira, kukuza kipato cha wananchi na kuchochea maendeleo ya uchumi nchini.
Aidha, amesema Serikali inalenga kuimarisha biashara kwa kutumia Mikoa ya mipakani kama vituo muhimu vya masoko katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Amesema maeneo ya mipakani kama Tarime, yana nafasi ya kimkakati katika kukuza biashara kutokana na ukaribu wake na nchi jirani ya Kenya.
Londo amebainisha kuwa Serikali imeweka mkakati wa kuvutia uwekezaji kupitia vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi, hususan kwa miradi ya kimkakati inayoweza kuanzishwa katika maeneo maalum ya kiuchumi. Vivutio hivyo vinajumuisha misamaha na nafuu ya kodi ili kuhamasisha wawekezaji wakubwa kuwekeza nchini.
