Habari
MAAFISA BIASHARA WASISITIZWA KUWA WAWEZESHAJI BIASHARA DIRA 2050
Serikali imeendelea kuwasisitiza Maafisa Biashara Nchini kuwa wawezeshaji wa wafanyabiashara badala ya kuwa wadhibiti ili kufanikisha Dira ya Taifa 2050.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Prof. Neema Mori 18 Agosti 2026 akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Waziri Salum wakati akifunga Kikao Kazi cha siku mbili cha Wizara na Maafisa Biashara Nchini kilichofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.
Aidha, akisoma hotuba ya Katibu Mkuu, Prof. Mori aliwaelekeza maafisa biashara hao kurahisisha utoaji wa leseni, kusimamia Mabaraza ya Biashara na kuwaunganisha wafanyabiashara na taasisi kama BRELA, TBS, SIDO na TANTRADE huku akiitaka mikoa kukamilisha kongani ya viwanda angalau kwenye wilaya moja.
“Leo tumekuja hapa tukiwa na malengo ya kutathmini utendaji wetu na kubainisha changamoto, tumethibitisha tena kwamba Dira ya Taifa 2050 na Ilani ya CCM 2025 hazitafikiwa kwa maneno bali kwa vitendo, alisema Prof. Mori
Akizungumza kuhusu shughuli 15 za biashara zilizokatazwa kwa wageni na kuhifadhiwa kwa Watanzania, Prof. Mori amewaelekeza pia Maafisa Biashara kuzitekeleza kwa haki na uwazi huku akibainisha kuwa timu ya Wizara kwa kushirikiana na BRELA itapita mikoani kufanya tathmini ya utekelezaji wa katazo hilo.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa amewasisitza Maafisa Biashara Nchini kuwajibika ipasavyo katika nafasi zao kwa kuwawezesha, kuwashauri na kuwapa wafanyabiashara miongozo sahihi ya biashara.
Nao baadhi ya Maafisa Biashara walioshiriki kikao hicho walieleza kuwa kutekelezwa kwa maelekezo yaliyotolewa na Wizara kutasaidia udhibiti wa bidhaa bandia sokoni na kulinda mitaji ya wafanyabiashara dhidi ya ushindani usio wa haki sokoni.
