Habari
WADAU WAARIKWA KUHUDHURIA KONGAMANO LA 25 LA UTAFITI NA BIASHARA KUHUSU USHINDANI WA VIWANDA NA BIASHARA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Doto James awaarika wadau mbalimbali kuhudhuria kongamano la 25 la utafiti na biashara kuhusu ushindani wa viwanda na biashara linalotarajiwa kufanyika Dar es salaam mwezi Novemba mwaka huu.
Katibu Mkuu Doto James ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza kuhusu kongamano hilo la 25 litakalofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu, Julius Nyerere uliopo jijini Dar es Salaam na kufunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango.
Kongamano hilo la 25 la utafiti na biashara kuhusu ushindani wa Viwanda na Biashara lililobeba kauli mbiu “Mapinduzi ya uchumi wa Tanzania kupitia Ushindani wa Viwanda na Biashara” ambayo inafungamana na mpango wa tatu wa maendeleo wa miaka mitano unaosisitiza kuendeleza juhudi za kuleta mageuzi ya kiuchumi, kuimarisha ushindani wa kitaifa na kuboresha maendeleo ya watu.
Kongamano la 25 la Utafiti na Biashara kuhusu ushindani wa Viwanda na Biashara linatarajiwa kufanyika Novemba 10, mwaka huu huku Mzungumzaji Mkuu akitarajiwa kuwa Mwanauchumi mashuhuri wa Kimataifa Prof. Justin Yifu Lin.
Prof. Lin ni mwanzilishi wa Taasisi ya Misingi mipya ya uchumi katika Chuo Kikuu cha Peking na amewahi kuwa Mchumi Mkuu wa Benki ya Dunia (WB).
Bw. Doto James Amesema kuwa kongamano hilo lenye lengo la kuchochea na kukuza mijadala ya kisera na utafiti kuhusu viwanda na biashara kama sekta muhimu ya kuharakisha ukuaji wa uchumi na kichocheo cha mabadiliko ya kimuundo litahudhuriwa na washiriki 200 ambapo watakuwepo viongozi wakuu kutoka Serikali ya Tanzania na Mapinduzi ya Zanzibar, na kutokana na sababu ya vikwazo vya usafiri waalikwa kutoka nje ya nchi watashiriki kwa njia ya mtandao.
Bw. Doto James Ameongeza kwa kusema kuwa mabadiliko ya muundo wa uchumi ni muhimu katika kutengeneza ajira zinazohitajika kwa vijana, kupunguza umaskini, na kuimarisha ustahimilivu wa kiuchumi dhidi ya majanga mbalimbali.
“Viwanda na biashara shindani ndio vichocheo muhimu vya mabadiliko ya kimuundo na ukuaji. Hii inaelezea ushirikiano unaoendelea kati ya Wizara ya Viwanda na Biashara na REPOA kwa warsha hii na programu nyingine za utafiti na kujenga uwezo juu sekta hizi.” Alisema.
Bw. Doto James Amesema kuwa kongamano hilo linaloandaliwa na REPOA na kufanyika kila mwaka huwakutanisha watafiti, wabobezi, watunga sera, washirika wa maendeleo, AZAKI, Sekta binafsi na wasomi kutoka taasisi za elimu ya juu ndani na nje ya nchi ili kujadili masuala ya maendeleo, matokeo ya tafiti kutoka kwa watafiti waliobobea ili yasaidie kuboresha sera na kuchangia kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kuboresha maisha ya watanzania.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa REPOA, Dkt. Donald Mmari alisema makongamano yaliyofanyika siku za nyuma yameleta mchango mkubwa kwa taifa na sekta ya viwanda na biashara kwa ujumla.
Dkt. Mmari ameongeza kwa kusema kuwa makongamano haya ya mesaidia Serikali kuboresha mifumo ya kiutendaji katika kuwafikia wananchi na kutatua changamoto zinazowakabili.