Habari
Watanzania changamkieni fursa ya kuwania Tuzo za Ubora za Kitaifa 2022/2023

Watanzania wametakiwa kuchangamkia fursa ya kuwania Tuzo za Ubora za Kitaifa kwa mwaka 2022/2023 ambazo zinahusisha Sekta mbalimbali na watu binafsi wanaofanya vizuri kwenye masuala ya Ubora ambazo zitasaidia kuitangaza nchi.
Akizungumza na Vyombo vya Habari Oktoba 27, 2022 Jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Tuzo Tatu za Ubora za Kitaifa Mwaka 2022/2023 Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Bw Aristides Mbwasi amesema kuwa tuzo hizo zitaleta fursa katika kuendeleza na kukuza Sekta ya Viwanda na Biashara.
Amesema mashindano ya Tuzo hizo yamegawanyika katika Tuzo kwa kampuni bora , tuzo kwa bidhaa bora , tuzo kwa huduma bora , tuzo kwa muuzaji bora wa bidhaa nje ya nchi na mtu mmoja aliyefanya vizuri kwenye masuala ya ubora .
Pia amesema katika mashindano hayo wadau watapata fursa ya kufahamika zaidi kwenye jamii na kushiriki kwenye Mashindano ya tuzo za ubora kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mashindano ya tuzo za ubora kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na hivyo kupata fursa za masoko.
Aidha, amesema Serikali kupitia Wizara ya Uwekezaji ,Viwanda na Biashara iliona umuhimu wa kuanzisha tuzo hizi na kutoa jukumu la kuziratibu kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) na Shirika la Viwango Zanzibar pamoja na Shirikisho la wenye Viwanda nchini (CTI ).
Pia Bw. Mbwasi ametaja Taasisi ziningine zilizoshirikishwa ni pamoja na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo nchini (SIDO) ,Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Chemba ya Wafanya Biashara, Wenye Viwanda na Kilimo Tanzania(TCCIA) na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE).
Hata hivyo aliwataka watanzania kuwa mabalozi wa kuhamasisha wazalishaji wa bidhaa na watoa huduma kushiriki mashindano ya Tuzo za ubora za mwaka 2022/2023.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania Dkt Athuman Ngenya akizungumzia maandalizi ya Tuzo hizo amesema kuwa maandalizi yanaendelea vizuri na wanatumia warsha mbalimbali, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ili kusaidia kuwapata washindi.
"Katika maandalizi haya tumewapa kipaumbele akina mama wajasiliamali kuwahamasisha ili waweze kushiriki kwani ni wengi ambao wamejikita kwenye ujasiliamali." Alisema Ngenya.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Viwango Bi. Hafsa Ali Slim
akimuwakilisha Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Zanzibar (ZBS) amesema kuwa wanatarajia kutoa uelewa kwa wafanyabiashara na wazalishaji wa bidhaa mbalimbali kwa upande wa Zanzibar ili waweze kushiriki kwa wingi zaidi.